Akiba Haiozi?
Leo tutajaribu kupima ukweli na tafsiri halisi ya msemo wa "akiba haiozi." Huenda huu msemo una maana tofauti na viashiria tofauti katika karne hii ya 21.
Akiba ni kiasi cha pesa kinachowekwa pembeni, au nje ya matumizi, kwa malengo ya baadaye. Kuna namna nyingi za kuweka akiba kama vile kwa kutumia kibubu, akaunti ya benki, nk. Hata hivyo, usahihi wa "akiba haiozi" utaamuliwa na vitu viwili muhimu. Kitu cha kwanza ni njia unayotumia kuweka akiba, na kitu cha pili ni malengo ya kuweka akiba.
Akiba inaweza kuoza endapo utatumia njia zisizo sahihi kuweka akiba. Vilevile, akiba inaweza kuoza endapo hauna malengo ya msingi ya kuweka akiba.
Ukiweka akiba katika kibubu, akiba yako itaoza katika namna kadhaa. Namna mojawapo ni mfumuko wa bei. Pesa yako itapungua thamani kadri muda unavyokwenda, na hivyo kuwa na uwezo mdogo wa kukidhi mahitaji yako. Namna nyingine ni usalama mdogo wa pesa. Njia ya kuhifadhi kwenye kibubu inaiweka pesa yako katika hatari kama vile wizi au kuungua kwa moto. Hivyo basi, endapo utaweka akiba kwa kupitia njia hii, akiba itaoza.
Ukiweka akiba katika akaunti ya benki, akiba yako inaweza kuoza kutegemea na aina ya akaunti unayotumia. Akaunti ya kawaida inafanya akiba yako ioze. Kuna makato ya mwezi, makato ya kadi, makato ya miamala, nk. Lakini pia mfumuko wa bei upo palepale, kwahiyo akiba yako itaoza kwa kasi! Endapo ukiwa mjanja ukafungua akaunti maalumu ya akiba (savings account) utakuwa na nafuu. Hata hivyo, ongezeko la kila mwezi linaweza kuwa kidogo na kushindwa kufidia madhara ya mfumuko wa bei kikamilifu. Faida ya kutumia akaunti ya benki kulinganisha na kibubu ni usalama wa pesa yako.
Ukiweka akiba katika akaunti za mitandao ya simu, akiba yako inaweza kuoza kutokana na mfumuko wa bei pamoja na gharama za miamala.
Kuhusu malengo ya kuweka akiba ni kwamba huna budi kuwa na mipango kuhusu akiba unayoweka. Watu wengi wanaweza kuweka akiba, lakini si ajabu kumkuta mtu ananunua nguo kwa kutumia pesa ya akiba. Watu wengi bado hawana dhana ya uwekezaji. Ni vyema ukaweka akiba kwa malengo ya kufanya uwekezaji, na sio matumizi. Ukitumia pesa ya akiba kufanya manunuzi ya kitu kisichozalisha pesa zaidi, hiyo ni sawa na kwamba akiba yako imeoza. Ni kana kwamba uliamua kuahirisha matumizi sasa ili ufanye matumizi baadaye!
Endapo una nia ya kuona jinsi gani akiba haiozi, kuwa makini na njia unazotumia kuweka akiba, jifunze kuhusu uwekezaji, na ujiwekee malengo ya kufanya akiba yako izalishe pesa zaidi. Sio lazima pesa uliyoweka akiba izalishe pesa nyingi. Endapo akiba yako inaongezeka kwa kasi sawa na kasi ya mfumuko wa bei, hapo akiba yako ipo salama.
Baadhi ya namna za kuweka akiba ili akiba yako isioze ni kama vile: amana za benki (fixed deposits), mifuko ya uwekezaji wa pamoja (mutual funds), kununua mali inayopanda thamani, nk. Badili mtazamo kuhusu kuweka akiba, na utapata faida za kuweka akiba. Jifunze kuwekeza akiba unayoweka. Unaweza kuanza uwekezaji muda wowote bila kujali kipato chako ni kidogo au kikubwa. Kama una nidhamu ya kutenga pesa pembeni bila kuitumia, ongezea na elimu ya uwekezaji ili uvune matunda ya akiba yako.
Katika siku zijazo tutazidi kujifunza kuhusu njia bora za kuweka akiba na uwekezaji kwa ujumla. Kwa sasa tuishie hapo.