Collective Investment Schemes Pt. 2

Collective Investment Schemes Pt. 2
Mutual Funds

Karibu tena tuendelee kujifunza kuhusu mifuko ya uwekezaji wa pamoja, collective investment schemes. Baada ya kujifunza juu ya maana, aina na umuhimu wa mutual funds, tuangalie vitu vya kuzingatia kabla ya kuwekeza katika mutual funds.

Vitu vya kuzingatia kabla ya kuwekeza.

  1. Hakikisha umesoma chapisho liitwalo OFFER DOCUMENT ambalo linaelezea kuhusu mfuko husika. Ndani ya offer document utapata kujua vitu kama vile sera ya uwekezaji (investment policy), mfumo wa uongozi, historia kuhusu mfuko husika, kiwango cha chini cha uwekezaji, nk.
  2. Fuatilia utendaji wa mfuko kupitia kusoma ripoti ya mwaka (annual report) na ripoti za kifedha (financial statements). Hapa unaweza kupata picha juu ya mwenendo wa mfuko, na kama ni sahihi kuwekeza huko.
  3. Fuatilia gharama za uendeshaji (operational costs) za mfuko husika. Endapo gharama za uendeshaji ni zaidi ya 5% ya mtaji (net asset value) wote, huo mfuko una gharama kubwa na hupaswi kuwekeza huko.
  4. Kama ni mfuko mpya, fuatilia kama wamepata kibali kutoka kwa mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana, CMSA. Kwa mfano siku ya tarehe 9 Julai 2024 Sanlam Investments walianzisha mifuko miwili ya uwekezaji wa pamoja, kwa idhini ya CMSA. Kama CMSA hawajatoa idhini, huo mfuko sio salama kuwekeza pesa zako.
  5. Kama ni mfuko mpya, fuatilia historia ya viongozi wa mfuko (fund managers) ili kujua kama wana uzoefu wa kutosha katika uwekezaji. Usiwe na upesi kuwekeza kwa sababu ni mfuko mpya.
  6. Fuatilia namna za kuwasiliana na wahudumu (customer service) endapo utapata changamoto. Fuatilia kama wana ofisi jirani na unapoishi. Fuatilia kama wana namba ya simu au baruapepe, na pia kama wanapatikana kiurahisi kwa njia hizo.
  7. Fuatilia website yao na machapisho kama vile vipeperushi. Ukiweza nenda katika ofisi zao ili wakupe ufafanuzi juu ya mfuko au mifuko wanayosimamia.
  8. Angalia njia mbadala za kuwekeza, kama zipo. Huenda unaweza kupata faida kubwa kupitia aina nyingine za uwekezaji kama vile kununua hisa, bonds, au kufanya biashara mwenyewe. Jaribu kupima machaguo mengi tofauti kabla ya kuamua kuwekeza katika mutual funds.
  9. Fuatilia utaratibu wa kurudishiwa pesa zako inapotokea dharura. Fuatilia muda unaopita kabla ya kupata pesa zako. Fuatilia njia za miamala zinazotumiwa na mfuko husika.

Hayo hapo juu ni baadhi ya mambo muhimu kuzingatia kabla ya kuanza kuwekeza katika mutual funds. Uwekezaji unahitaji kuwa makini sana mwanzoni, lakini kazi inakuwa ndogo baadaye.

Cha muhimu zaidi kuzingatia katika uwekezaji ni kufuata kanuni ya uwekezaji mseto (diversification). Jitahidi kugawanya pesa zako katika vyanzo tofauti tofauti vya mapato (multiple streams). Inapotokea chanzo kimoja hakifanyi vizuri, bado unaweza kupata pesa kupitia vyanzo vingine. Kwa mfano, unaweza kununua hisa kiasi, bonds kiasi, na vipande kiasi, kwa kuzingatia asilimia fulani ya mtaji wote.

Siku nyingine tutachambua sifa za baadhi ya mutual funds zinazofanya vizuri Tanzania, kama vile mfuko wa Ukwasi wa UTT AMIS. Kwa leo nikuache na swali kwa ajili ya tafakari na majadiliano. Je, kama unaweza kupata faida kubwa kupitia biashara, kuna haja gani ya kufanya uwekezaji?

Read more