Dhamana za Muda Mfupi (Short-term Securities).

Dhamana za Muda Mfupi (Short-term Securities).
Money Market

Karibu tena tuendelee kujifunza. Siku ya leo tutaangalia vitu kadhaa kuhusu dhamana za muda mfupi. Hapa tunaongelea hati zenye ukomo chini ya mwaka mmoja, ambazo kwa ujumla hupatikana katika soko liitwalo "money market." Kwa Kiswahili tunaweza kusema soko la fedha.

Money market pamoja na capital market kwa ujumla hujulikana kama "financial market." Kuhusu capital market tuliona kwamba ni soko la dhamana au hati za muda mrefu, zaidi ya mwaka mmoja, kama vile hisa, vipande na hatifungani za muda mrefu (bonds). Kwa upande wa money market, tunaongelea dhamana kama vile amana za muda maalumu za benki (fixed deposit), hatifungani za serikali za muda mfupi (treasury bills), fedha za kigeni (forex), amana za makampuni (commercial papers), nk.

Dhumuni kubwa la dhamana za muda mfupi ni kutosheleza mahitaji ya muda mfupi ya mtaji. Kampuni ama mtu binafsi hununua dhamana za muda mfupi kwa ajili ya kupunguza hatari za kifedha, kama vile kupotea kwa mtaji. Zinatumika dhamana hizi kwa sababu mmiliki anakuwa na matarajio ya kurejesha pesa zake ndani ya muda mfupi, tofauti na ilivyo kwa hati za muda mrefu. Mfano mzuri ni inapotokea kampuni imeweza kupata faida kubwa ndani ya muda fulani. Wanaweza kuwekeza pesa hizo katika dhamana za muda mfupi, kana kwamba wataweza kuepuka kupoteza thamani kutokana na mfumuko wa bei. Kitu kingine hapa ni kwamba kuna hatari ndogo katika hati hizi kuliko za muda mrefu (less risky).

Tuanze kwa kuangalia hatifungani za muda mfupi za serikali, treasury bills. Hizi ni dhamana zitolewazo na serikal ya Tanzania kupitia benki kuu, BOT. Ni namna ya serikali kukopa pesa kwa umma kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kuboresha uchumi kwa kudhibiti mzunguko wa fedha (money supply). Treasury bills zina ukomo wa siku 364, siku 182, siku 91 na siku 35. Muda wa ukomo ni chini ya mwaka mmoja. Treasury bills na treasury bonds huuzwa kupitia mnada wa BOT unaofanyika kila wiki siku ya Jumatano. Huwa kuna utaratibu wa kupokezana kwa wiki. Wiki hii ikiwa treasury bonds, wiki inayofuata ni treasury bills.

Katika mnada wa treasury bills, kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 500,000. Utaratibu ni kwamba unaomba kununua hati kwa bei ambayo ipo chini ya 100% ya bei halisi. Kama bei halisi ni TZS. 1,000,000 hapo unaomba kununua labda kwa bei ambayo ni 97% ya hiyo milioni moja. Hii ina maana kuwa utalipa TZS. 970,000 kununua treasury bills zenye thamani ya milioni moja. Baada ya muda wa ukomo, utalipwa milioni moja. Faida yako ni TZS. 30,000. Kiwango cha faida inategemea na bei uliyonunulia mwanzoni, ambayo huamuliwa na ushindani katika mnada husika.

Kama wewe upo tayari kulipa 95% ya bei, na watu wengi wapo tayari kulipa zaidi ya hapo, labda 96.5%, una uwezekano wa kukosa treasury bills katika mnada huo. Wingi wa watu ambao wapo tayari kulipa asilimia fulani ya bei ndio kigezo cha kuamua treasury bills ziuzwe katika asilimia ngapi ya bei. Katika mfano wetu, watu wanaolipa 96.5% au zaidi watapata treasury bills.

Faida ipatikanayo kupitia treasury bills sio kubwa, lakini ni ya uhakika na unapata ndani ya muda mfupi. Mara nyingi faida huwa haifiki hata 5% ya mtaji.

Tuishie hapo kwa sasa. Wakati ujao tutaendelea tulipoishia, kufafanua zaidi kuhusu hizi dhamana za muda mfupi.

Read more