Elimu ya Fedha.
Karibu tena ndugu msomaji. Siku ya leo tujifunze kuhusu elimu ya fedha kwa ujumla wake, na kwa nini elimu hiyo ni muhimu kuwa nayo.
Elimu ya fedha ni ujuzi wa kuzalisha pesa, kutunza pesa, kugawanya pesa katika matumizi mbalimbali, na kuwekeza pesa ili kuzalisha pesa zaidi. Kuna vitu vinne muhimu katika elimu ya fedha, kama inavyoonekana katika tafsiri tajwa hapo juu.
Kwa kuanza na upande wa kuzalisha pesa, hapa tunaongelea kuwa na ujuzi wa kuingiza kipato kwa njia halali aidha kwa kujiajiri ama kuajiriwa. Watu wengi hutumia muda wao zaidi katika kujifunza ujuzi wa namna hii. Wapo wanaosoma shule miaka mingi ili kupata ujuzi wa kuzalisha pesa kupitia taaluma (profession) zao. Wapo wanaojifunza kuzalisha pesa kupitia uanagenzi (apprenticeship) chini ya watu wenye uzoefu zaidi. Hizo ni njia mbili za kujifunza ujuzi wa kuzalisha pesa. Ndizo zinazotumiwa zaidi.
Kwa bahati mbaya, kuna watu ambao taaluma zao hazina uwezo wa kuzalisha pesa kutokana na kukosekana kwa ajira. Watu hawa ni wengi na hulazimika kutafuta pesa kwa kutumia ujuzi tofauti na taaluma zao. Kulingana na ujuzi unaohitajika, wengine hujifunza kupitia uanagenzi, kozi za mitandaoni, nakadhalika.
Katika eneo la ujuzi wa kuzalisha pesa tunaona kwamba wengi wana ujuzi huo, na wanaendelea kufuatilia ili kujua zaidi.
Eneo la pili la elimu ya fedha ni ujuzi wa kutunza pesa. Kwa bahati mbaya, elimu hii haipatikani shuleni. Hivyo mtu analazimika kujifunza kwa namna nyingine kama vile kusoma vitabu, kuhudhuria semina, nk. Watu wengi hawana ujuzi huu kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi wanajua kwamba ni muhimu kutunza pesa, lakini hawajui waanzie wapi. Wengine wanaamini pesa wanazopata ni kiduchu mno. Ukweli ni kwamba ujuzi wa kutunza pesa ni muhimu sana katika kutafuta uhuru wa kifedha.
Sehemu ya tatu ya elimu ya fedha ni kugawanya pesa katika matumizi mbalimbali (budgeting). Kutokana na kwamba tunatumia jitihada kubwa kuzalisha pesa, ni dhahiri pia kwamba kuna haja ya kupangilia matumizi vizuri. Elimu hii pia haipatikani shuleni, na ndio maana kuna wasomi wengi wasiokuwa na elimu hii. Hata kama una ujuzi wa kutunza pesa, ukishindwa kupangilia matumizi vizuri, hata akiba yako itabadilika kuwa pesa ya matumizi.
Sehemu ya nne ya elimu ya fedha ni ujuzi wa kuwekeza pesa ili kuzalisha pesa zaidi. Ukweli ni kwamba binadamu hatuna uwezo wa kufanya kazi muda wote maishani mwetu. Kuna kuumwa, kupata ajali, kustaafu, nk. Ni vyema kuwa na ujuzi wa kuwekeza pesa tunazopata katika shuguli zetu za uzalishaji. Elimu hii inapatikana shuleni, lakini sio kila mtu hupata nafasi ya kusomea mambo ya fedha na uwekezaji. Kuna watu wanasoma masuala ya upangishaji majengo (real estate), masoko ya mitaji (capital markets), nk. Wengine hupata elimu hii kupitia vitabu, semina, uanagenzi, nk.
Elimu ya uwekezaji ni muhimu sana kwa sababu inao uwezo wa kukuondolea ulazima wa kufanya tena shughuli za uzalishaji. Watu wengi hawana elimu hii. Chini ya asilimia moja (1%) ya watanzania wanawekeza katika masoko ya mitaji. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya kuwa na elimu ya uwekezaji na kuwa na uhuru wa kifedha.
Bila kuwa na elimu ya uwekezaji, watu hulazimika kufanya kazi miaka mingi bila kuona mabadiliko yoyote katika ubora wa maisha yao. Wengine huwaza kuongeza ujuzi wa kuzalisha pesa ilihali hawajui chochote kuhusu uwekezaji. Ndio maana utakutana na wafanyakazi wanaongeza elimu ili kuongezewa mishahara. Ni kitu kizuri, lakini wengi wao hawafikirii kwamba kuna siku watashindwa kufanya kazi kwa sababu mbalimbali.
Elimu ya fedha kwa ujumla wake ni elimu muhimu sana. Ni elimu ambayo kila mtu anahitaji kuwa nayo, kwa sababu hatuna uwezo wa kukwepa kutumia pesa. Kama mtu ana matumizi makubwa kuliko kipato chake, madeni hayaepukiki na huo ni mtego mbaya sana. Watu wengi wanaingia kwenye madeni "kausha damu" kwa kukosa elimu ya fedha. Kwa hali kama hii, uhuru wa kifedha utabaki kuwa ndoto, tena ndoto ya mchana.
Ili andiko lisiwe refu, naamua kuishia hapa kwa sasa. Tukutane wakati ujao kwa elimu zaidi. Elimu ya fedha ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya adui umasikini.