Hasara Katika Uwekezaji (Losses in Investing)

Hasara Katika Uwekezaji (Losses in Investing)
Losses in Investing

Karibu tena katika blog yetu mpendwa msomaji. Siku ya leo tutagusia kuhusu hasara zinazoweza kupatikana katika uwekezaji, haswa upande wa masoko ya mitaji (capital markets). Tayari tuna upeo kiasi fulani juu ya mapato ya aina mbalimbali katika uwekezaji, ikiwemo gawio na ongezeko la thamani ya mtaji. Hata hivyo, sio kila wakati tutapata faida tu. Kuna nyakati kadhaa ambapo mtu hupata hasara katika uwekezaji.

Uwezekano wa kupata hasara unaweza kupungua, lakini sio kuondolewa kabisa. Hakuna mwekezaji anayepata faida muda wote, bila kupata hasara hata mara moja. Miongoni mwa visababishi vya hasara hizo ni kutokuwa na picha kamili juu ya mambo yajayo. Katika uwekezaji tunajaribu kutabiri kuwa thamani ya mtaji itapanda endapo tukiwekeza katika mradi fulani. Ukweli ni kwamba hata kama tunao ushahidi wa kutosha kuhusu uwezekano wa faida, hatuna uhakika kama kweli faida itapatikana.

Hasara mojawapo inayoweza kutokea katika uwekezaji ni kupotea kwa thamani ya mtaji (capital loss). Badala ya thamani ya mtaji kuongezeka kama tunavyotegemea, inatokea kinyume chake. Thamani ya mtaji inashuka na kuwa chini hata ya ilivyokuwa wakati wa kuwekeza. Upotevu huu wa thamani unaweza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa ubora wa utendaji kazi hivyo kupelekea kupungua kwa mapato ya kampuni. Kupungua kwa mapato hupelekea kushuka kwa pato la kila hisa (earning per share, EPS) pamoja na kushuka ama kuondolewa kwa gawio. Mapato yanaweza kushuka kiasi cha kuzalisha hasara badala ya faida kwa kila hisa unayomiliki. Hali hii husababisha hata bei ya hisa sokoni kushuka kutokana na mtazamo wa wanunuzi wa hisa.

Kama umeamua kuuza hisa kwa bei ndogo kuliko bei uliyonunulia mwanzoni, hasara hii ya upotevu wa mtaji hutokea. Lakini usipouza hisa zako, bado hauna hasara. Hata hivyo, uwekezaji wako unakuwa umepungua nguvu ya kuzalisha faida hadi kufikia kiwango cha kushuka kwa EPS na gawio.

Hasara nyingine inayoweza kutokea katika uwekezaji ni kushindikana kulipwa riba katika hatifungani za muda mrefu (bonds). Hali hii inaweza kutokea endapo taasisi husika inayopaswa kulipa riba imefilisika (bankrupt). Kama unamiliki bonds za kampuni halafu hiyo kampuni ikafilisika, hautaweza kulipwa riba wala kiwango cha mwanzo ulichotoa kuikopesha hiyo kampuni.

Katika upande huohuo wa bonds, inawezekana pia mfumuko wa bei ukawa kiwango kikubwa kiasi cha kuondoa sehemu kubwa ya riba unayopaswa kulipwa. Hata thamani ya pesa ulizotoa kukopesha inashuka sana endapo kuna kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei. Unaweza kuambulia faida kiduchu sana kutokana na athari hizi za mfumuko wa bei. Athari za mfumuko wa bei hazitabiriki, lakini zipo na zinaweza kusababisha hasara katika uwekezaji.

Namna pekee ya kuepuka hasara katika uwekezaji ni kuepuka uwekezaji kabisa. Tunatamani kupunguza hasara katika uwekezaji, lakini kutokomeza hasara kabisa ni jambo lililo nje ya uwezo wetu. Ili tuweze kupunguza hasara katika uwekezaji, hatuna budi kufanya uchambuzi na utafiti wa kina kabla ya kuwekeza pesa zetu. Kuwa makini na mtu anaesema hajawahi kupata hasara katika uwekezaji, na ujiulize kwanini ameamua kusema hivyo. Endapo tukiwa wawekezaji makini, tutapata matokeo mazuri katika uwekezaji, kwa maana ya kupata faida kubwa na endelevu, na kupunguza hasara kwa kiasi kikubwa.

Mpaka hapo tumefikia tamati ya andiko hili la siku ya leo. Tukutane wakati mwingine ili tuzidi kujifunza mambo mbalimbali kuhusu uwekezaji. Karibu sana.