Hatari Katika Uwekezaji (Investment Risk).
Karibu tena ndugu msomaji na mwekezaji. Leo tutajifunza kuhusu hatari (risks) zilizopo katika uwekezaji. Ni sehemu muhimu sana katika uwekezaji, hivyo ni vizuri kama una uelewa mpana wa dhana hii.
Katika uwekezaji kuna hali ya sintofahamu (uncertainty) wakati wote. Mtu hauna uhakika kama utapata faida au hasara, na kwa kiwango gani. Mtu hauna uhakika kama fursa uliyochagua ina tija zaidi ya fursa ulizoacha. Hauna uhakika kama umewekeza kiwango cha kutosha cha fedha ili kuweza kupata faida kubwa. Kiufupi kunakuwa na mambo mengi ambayo yanabadilika kiurahisi na ni ngumu kujua majibu sahihi. Ndio maana tunasema kwamba kuna hatari katika uwekezaji.
Mara nyingi unakuwa na uwezo wa kupata faida kulingana na kiwango cha hatari katika uwekezaji unaofanya. Hatari kubwa huambatana na faida kubwa, kadhalika hatari ndogo huambatana na faida ndogo. Mfano wa uwekezaji wenye hatari kubwa ni kumiliki hisa za kampuni. Kuna hatari ya kushuka kwa bei ya hisa hivyo kupoteza thamani ya uwekezaji wa mwanzo. Lakini pia kumiliki hisa ni mojawapo ya njia bora za kutengeneza utajiri.
Mfano wa uwekezaji wenye hatari ndogo ni kumiliki hatifungani za serikali. Hata hivyo, uwekezaji huu sio njia bora sana ya kutengeneza utajiri. Uwekezaji wenye hatari ndogo unafaa zaidi endapo mtu tayari ana kiasi kikubwa cha fedha, sio kwa mtu anayetafuta kuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Kitu kingine cha kuangalia ni utayari wa mwekezaji kushiriki katika uwekezaji wenye hatari kubwa au ndogo. Hii inajulikana kama "risk appetite." Wapo wenye utayari mkubwa wa kuwekeza katika miradi yenye hatari kubwa, na wanaitwa "enterprising investors." Wapo pia watu wenye utayari mdogo wa kuwekeza katika miradi ya namna hiyo, na wanaitwa "defensive investors." Kila mmoja anahitajika kuwa tayari kuwekeza kwa kiwango fulani katika miradi yenye hatari kubwa, na kiwango fulani katika miradi yenye hatari ndogo.
Faida ya kuwekeza katika miradi yenye hatari kubwa ni uwezekano wa kupata faida kubwa. Faida ya kuwekeza katika miradi yenye hatari ndogo ni kuwa na uhakika wa kipato, na kulinda thamani ya uwekezaji wa mwanzo. Mtu yeyote ni vizuri awekeze katika miradi ya aina zote mbili, kwa asilimia maalumu kulingana na hatua aliyopo kiuchumi, na utayari wake pia.
Endapo lengo la uwekezaji ni kutengeneza utajiri, ni vyema kuwekeza asilimia kubwa ya mtaji katika miradi yenye hatari kubwa, na asilimia inayobakia kwenye miradi yenye hatari ndogo. Kama lengo la uwekezaji ni kuwa na uhakika wa kipato, ni vyema kuwekeza asilimia kubwa ya mtaji katika miradi yenye hatari ndogo, na asilimia inayobakia katika miradi yenye hatari kubwa. Viwango halisi vinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.
Kigezo cha umri pia ni muhimu sana. Kijana hawezi kuwekeza kama mtu anayekaribia kustaafu. Ni vizuri mtu mwenye muda wa kutosha ajikite kuwekeza kwa malengo ya kutengeneza utajiri. Ni vizuri pia mtu mwenye muda mfupi ajikite kuwekeza kwa malengo ya kupata uhakika wa kipato. Hii ni kutokana na makadirio ya miaka ya kuishi (life expectancy).
Baada ya kujifunza mambo machache kuhusiana na hatari katika uwekezaji, ni vyema kujiwekea mipango madhubuti ya uwekezaji. Ni vizuri kama mtu utajipangia kabisa asilimia maalumu za kuwekeza mtaji katika miradi mbalimbali ili kuwa na "portfolio." Kumbuka kwamba unapotaka kutengeneza utajiri kupitia uwekezaji, unahitaji muda wa kutosha.
Tukutane tena wakati mwingine ili tuzidi kujifunza mambo muhimu katika uwekezaji. Nikutakie heri katika uwekezaji wako.