Hisa vs. Hatifungani
Karibu tena ndugu msomaji. Leo tujadili kidogo kuhusu tofauti, ufanano, faida, na hata hasara pia; katika uwekezaji upande wa hisa (shares) na hatifungani (bonds).
Awali ya yote, hisa ni nini? Hisa ni hati inayokupa haki ya kumiliki sehemu ya mali na mapato ya taasisi fulani, sanasana kampuni.
Hatifungani ya muda mrefu (bond) ni hati inayokupa haki ya kulipwa riba maalumu (fixed coupon/interest) kila mwaka mpaka ufikapo muda wa ukomo wa hati (maturity), ambapo ukifika muda wa ukomo utalipwa pesa ya mwanzo (face value) uliyoikopesha taasisi husika.
Tofauti mojawapo kati ya hisa na bonds ni kwamba mtu anaemiliki hisa ni mmiliki wa kampuni, lakini mtu anaemiliki bonds ni mkopeshaji wa kampuni au taasisi husika. Hii inamaanisha kwamba mmiliki wa hisa ana haki ya kushiriki katika mikutano ya kampuni, kupiga na kupigiwa kura, nk. Mmiliki wa bonds anaidai taasisi pesa, na si vinginevyo.
Tofauti nyingine ni kwamba mmiliki wa bonds anapewa kipaumbele zaidi katika kulipwa pesa kuliko mmiliki wa hisa. Ni sawa na kusema wamiliki wa kampuni mnaweza kulipana pesa hata baadaye, lazima muanze na kulipa madeni. Hata taasisi ikipata hasara, mmiliki wa bonds anaendelea kudai pesa yake. Wamiliki wa kampuni hasara itawahusu kulingana na idadi ya hisa zenu. Hata hivyo, ukimiliki hatifungani za makampuni (corporate bonds), unaweza kupata hasara kama kampuni ikifilisika.
Tofauti nyingine ya msingi ni kwamba kiwango cha malipo kwa wanahisa kinabadilika kutokana na mambo mbalimbali, lakini kiwango cha malipo kwa mmiliki wa bonds hakibadiliki. Kiwango cha gawio kwa hisa moja (dividend per share) kinabadilika. Kiwango cha ongezeko la bei ya hisa moja (capital gain) kinabadilika. Lakini riba anayolipwa mmiliki wa bonds ipo palepale, kama ataendelea kumiliki hati aliyonayo.
Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba riba ya hatifungani (coupon rate) huwa inabadilika kutokana na maamuzi ya taasisi inayotoa hatifungani. Lakini ukishanunua bond yenye riba labda ya 15.95% kwa mwaka, utalipwa kwa riba hiyohiyo mpaka ukomo wa hati yako (maturity). Kwa mfano, riba ya bond ya miaka 25 ilikuwa 15.95% kipindi cha nyuma, lakini kwa sasa ni 12.56%.
Tofauti nyingine pia ni faida kwa mmiliki wa hisa. Ikitokea utendaji wa kampuni umeimarika na kuzalisha faida kubwa, mmiliki wa hisa atapata faida kubwa pia. Chukulia mfano wa mtu aliyenunua hisa za NMB kipindi inauzwa TZS. 3,020 mwaka 2023 mwanzoni, ambayo kwa sasa ninapoandika inauzwa TZS. 5,400. Ndani ya miezi 18 bei ya hisa imepanda kwa zaidi ya asilimia sabini! Hata gawio linatolewa kubwa zaidi kwa kila hisa moja endapo kampuni imepata faida kubwa. Mtu wa bonds anaendelea kulipwa kiasi kilekile.
Kitu kingine ni kiwango cha chini cha kuanza uwekezaji. Mara nyingi huwezi kuanza kununua bonds mpaka uwe na angalau TZS. 500,000. Hatifungani za serikali (treasury bonds) huwezi kununua kama pesa yako ni chini ya milioni moja. Kwa upande wa hisa, unaweza kuanza kununua hisa za AFRIPRISE hata ukiwa na shilingi elfu tatu! Kiwango cha chini katika kununua hisa ni idadi ya hisa, sio idadi ya noti na sarafu. Unaweza kuanza kwa kumiliki hisa kumi (10) tu. Ukiwa na hiyo laki tano au milioni moja unaweza kununua hisa nyingi sana.
Hasara moja ya kuzingatia katika kumiliki bonds ni kwamba kuna mfumuko wa bei (inflation). Kama umenunua bonds kwa milioni mia moja ili upate 15.95% kila mwaka kwa miaka 25, baada ya miaka 25 kuisha utalipwa milioni mia moja ileile. Mfumuko wa bei utafanya hiyo milioni mia moja iwe na thamani ndogo miaka 25 baadaye kulinganisha na hivi sasa. Hata hiyo milioni 15 unayolipwa kwa mwaka haitakuwa na thamani ileile miaka mitano baadaye.
Ufanano uliopo kati ya hisa na bonds sio wa muhimu sana, lakini wacha tugusie kidogo. Hisa na bonds zote ni mali unazoweza kubadili kuwa pesa kwa urahisi kulinganisha na mali nyinginezo kama ardhi. Hii ni hoja ya ukwasi (liquidity). Hoja nyingine ni kwamba unao uwezo wa kumiliki mali hizi bila kuonekana. Kuna faida ya kumiliki mali isiyoonekana (invisible wealth).
Mengine mengi kuhusu hisa na bonds tutazidi kujifunza wakati ujao. Ni elimu kama elimu nyingine, na elimu haina mwisho. Cha msingi zaidi ni kuendelea kuwa na kiu ya kujifunza. Karibu sana kwa maoni au maswali.