Intrinsic Value Pt. 2

Intrinsic Value Pt. 2
Intrinsic Value Pt. 2

Karibu tena katika blog yetu. Siku ya leo tutaendelea kujifunza kuhusu Intrinsic Value ya hisa, tukijikita zaidi katika namna ya kukokotoa Intrinsic Value. Lengo ni kutoa utangulizi wa namna ya kutumia Discounted Cash Flow Model (DCF) katika mahesabu hayo.

Kama tulivyoona katika andiko la mwanzo kuhusu Intrinsic Value, thamani halisi ya mtaji inapatikana kwa kukokotoa thamani ya sasa ya mtiririko wa fedha unaotarajiwa kupatikana katika uwekezaji. Katika kukokotoa thamani ya sasa, tunatumia kanuni ambayo ni kinyume na kanuni ya riba ambatani.

Katika upande wa riba ambatani, tunatafuta thamani ya uwekezaji baada ya muda fulani. Upande wa thamani halisi, tunatafuta thamani ya uwekezaji kwa sasa.

Ili tufanye hesabu hizi, tunahitaji kujua kiwango cha punguzo, Discount Rate (R). Kiufupi discount rate inaundwa na vitu viwili: riba ya chini kabisa inayoweza kupatikana kwa uhakika (kwa mfano riba ya hatifungani), pamoja na riba inayoweza kupatikana kutokana na kuhatarisha mtaji (risk premium). Katika mfano wetu tutakadiria riba ya hatifungani ni 10% na risk premium ni 10%. Jumla hapo tunapata discount rate ni 20% kwa mwaka.

Kitu kingine ni makadirio ya kiasi kinachoweza kupatikana baada ya muda, labda miaka mitano (5). Tunakiita kiasi hiki Future Cash Flow (FCF). Tukadirie FCF ni TZS. 25,000,000.

Ili kupata thamani ya sasa, ambayo ni Discounted Cash Flow (DCF) tunafuata hatua zifuatazo;

  1. Badili discount rate, R kuwa desimali kisha jumlisha na moja. 20% inakuwa 0.2 ambapo tukijumlisha na 1 inakuwa 1.2.
  2. Tafuta kipeo (power) cha discount rate kulingana na idadi ya miaka. Katika mfano wetu idadi ya miaka ni 5. Tukitafuta kipeo cha tano cha 1.2 tunapata 2.488 kwa nafasi tatu za desimali.
  3. Baada ya hapo, gawanya Future Cash Flow (FCF) kwa jibu la hatua iliyopita. FCF ni TZS. 25,000,000 na jibu la hatua iliyopita ni 2.488, ambapo tukigawanya tunapata TZS. 10,048,231.51 ambayo ndo thamani ya sasa (DCF). Kwahiyo Discounted Cash Flow (DCF) ni ndogo kuliko Future Cash Flow (FCF).

Hivyo tunaona dhahiri kabisa kwa kutumia njia hii ya DCF kwamba mtiririko wa fedha unaotarajiwa kupatikana una thamani ndogo kwa sasa kulinganisha na kiasi tunachotarajia.

Njia hii inatumika katika kuthaminisha mali za aina nyingi, ikiwemo hisa. Kwa upande wa hisa, ina aina kadhaa ikiwemo Discounted Dividend Model (DDM), Discounted Cash Flow to Equity (DCFE), pamoja na Discounted Cash Flow to Firm (DCFF). Njia hizi zote zinahitaji kanuni hii hii tuliyojifunza.

Kitu cha msingi kuzingatia ni kwamba hesabu hizi ni za makadirio na hazifanani kwa kila kampuni. Umuhimu mkubwa wa kufanya hesabu hizi ni kujiridhisha kwamba tunanunua hisa zenye Intrinsic Value kubwa. Andiko hili ni kama utangulizi tu, hivyo kuna haja ya kufuatilia zaidi endapo unataka kutumia maarifa haya katika kuthaminisha hisa (share valuation).

Kwa sasa tuishie hapo ndugu msomaji. Ni imani yangu kwamba utakuwa umejifunza kitu katika andiko la leo. Tukutane wakati mwingine ili tuendelee kujifunza. Karibu sana.