Kiwango cha Chini cha Kuweka Akiba.
Siku ya leo tutaangalia mambo machache kuhusu kuweka akiba. Watu wengi wanalalamika kwamba hawawezi kabisa kuweka akiba kwa sababu matumizi ni mengi mno. Kwamba "pesa haijawahi kutosha." Na madai mengine kama hayo. Ubaya wa haya mambo ni kwamba akili (Subconscious Mind) huwa na tabia ya kutafuta ushahidi (Manifestation) wa kuthibitisha kile unachoamini. Endapo imani yako ni potofu, akili itakupatia ushahidi wa imani hiyohiyo. Hii inasababisha mtu aendelee kuamini kitu kilekile hata kama sio sahihi.
Kama ni hivyo, hatuna budi kuanzia tatizo lilipo. Je, ni kweli kwamba pesa haijawahi kutosha? Kama ni kweli, tunaweza vipi kutenga fungu dogo kwa ajili ya akiba? Je, fungu hilo linatakiwa kuwa sehemu gani ya pesa zako zote? Katika kanuni za uchumi, pesa ni rasilimali. Ni rasilimali kwa sababu pesa hutumika katika uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali. Ni rasilimali adimu kwa baadhi ya watu, lakini kwa wengine pesa sio rasilimali adimu. Usemi wa pesa haijawahi kutosha una kiwango fulani cha ukweli. Hata hivyo, huna budi kuangalia namna za kujigawa hivyo hivyo.
Tabia moja ya matumizi ni kwamba hayana ukomo. Rasilimali zina ukomo, matumizi hayana ukomo. Huwezi kukidhi mahitaji yako yote bila kujali una rasilimali nyingi kiasi gani. Tunatumia hoja hii ili tutengeneze msingi wa kutenga fungu la akiba hata kama pesa haijawahi kutosha. Mahitaji ya msingi ya binadamu ni rahisi kuyatimiza kuliko "matamanio." Hapa tunaongelea mahitaji kama chakula, mavazi na makazi. Hapo zamani za kale binadamu alikuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji haya bila kuhitaji pesa. Kwa sasa ni ngumu kukidhi mahitaji ya msingi bila kuwa na pesa. Lakini haina maana kwamba utashindwa kabisa kukidhi mahitaji na kubakiwa na fungu dogo la kuweka akiba. Endapo utaangalia matumizi ya msingi zaidi na kuyafanya kuwa kipaumbele, utabaini kwamba kuweka akiba inawezekana kabisa.
Kuna kanuni inasema "A task will swell or contract in its perceived complexity according to the time allocated for its completion." Hii kanuni inaitwa Parkinson's Law. Kiufupi inamaanisha kuwa ugumu wa kazi utaongezeka ama kupungua kulingana na muda uliotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Kama umetenga muda mrefu wa kufanya jambo, utaliona kuwa ni jambo gumu kufanyika kwa kuamini kwamba "linahitaji muda mrefu." Sasa tujaribu kutumia kanuni hii kwa upande wa rasilimali pesa.
Tunaweza kusema, "Kuweka akiba kunaweza kuwa na ugumu ama wepesi kulingana na asilimia ngapi ya pesa zinapaswa kuwekwa akiba." Kama una mpango wa kuweka akiba asilimia kumi ya pesa zote, inaweza kuwa rahisi kuweka akiba kuliko mtu mwenye mpango wa kuweka akiba asilimia arobaini ya pesa zote. Lakini pia, "Matumizi ya pesa huongezeka ama kupungua kulingana na kiasi cha pesa ulichotenga kwa ajili ya matumizi." Kama umetenga kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya matumizi, lazima utakuwa na matumizi makubwa. Kama umetenga kiasi kidogo kwa ajili ya matumizi, utajikita kutumia pesa katika mahitaji ya msingi zaidi kulingana na pesa iliyopo. Tajiri na maskini wote wakila wali maharage wanashiba vilevile. Bajeti ya tajiri inaweza kuwa kubwa lakini mahitaji yake ya msingi hayahitaji pesa nyingi.
Kutokana na hoja zilizopita, tunaona kuwa: Kuweka akiba ni jambo linalowezekana kulifanya hata kama una pesa kidogo. Jambo lingine ni kwamba: Kuweka akiba ni rahisi endapo mtu anaweka akiba ambayo ni sehemu ndogo ya pesa zote. Kwa kuanzia, akiba inafaa kuwa asilimia kumi (10%) ya pesa zote. Kama una 50,000 ukatoa 5,000 kwa ajili ya akiba inamaanisha unabaki na 45,000 kwa ajili ya matumizi. Umejibana kiasi, lakini matumizi ya hiyo 45,000 yanaweza kuleta tija (utility) kubwa kwa sababu utajikita kutumia pesa katika mahitaji ya msingi zaidi. Ile 5,000 unakuwa umeiweka kama akiba, ambayo itakufaa wakati mwingine ukiwa na uhitaji. Ukitumia 50,000 yote, utakidhi mahitaji yako, lakini hautakuwa makini sana wakati wa kufanya manunuzi husika. Pesa itaisha, na utaendelea na mzunguko uleule wa kutafuta pesa na kuzitumia zote. Utakuwa unaamini pesa haijawahi kutosha na maisha yako yatakuwa ushahidi wa imani yako.
Binadamu haridhiki kiurahisi. Kutumia pesa nyingi hakuwezi kubadilisha kweli hii adhimu. Tengeneza utamaduni wa kutenga asilimia kumi ya pesa zote kwa ajili ya akiba. Hata ukitumia pesa zako zote, utaendelea kuwa na mahitaji yaleyale siku zijazo. Sasa kama utaendelea kuwa na mahitaji yaleyale siku zijazo, huoni kwamba ni busara kutenga fungu dogo kwa ajili ya matumizi ya siku hizo zijazo?
Naomba tuishie hapo kwa sasa ndugu msomaji. Huenda nimeandika maandishi tatanishi na maandishi chokozi/sumbufu kwa fikra zako. Jipe muda wa kutafakari ujue wewe binafsi una uwezo wa kutenga asilimia ngapi ya pesa zako kama akiba. Ni vyema iwe asilimia kumi au zaidi ya hapo, lakini isiwe asilimia kubwa sana. Mwisho wa siku lengo la kutafuta pesa ni kukidhi mahitaji, sio kuweka akiba. Tutakutana wakati mwingine ili tuzidi kujifunza pamoja kuhusu mambo haya ya kifedha.