Kodi ya Zuio (Withholding Tax).

Kodi ya Zuio (Withholding Tax).
Withholding Tax

Karibu tena ndugu msomaji. Kwa siku ya leo tutaifunza kiufupi kuhusu kodi ya zuio katika muktadha wa uwekezaji. Tutaangalia maana yake ni nini, na kugusia mifano ya uwekezaji ambapo kodi hii hukatwa au kutokatwa. Kwa kifupi inajulikana kama WHT kutokana na jina lake la Kiingereza.

Kodi ya zuio, WHT ni kodi inayokatwa katika mapato ya uwekezaji wako kabla hujaingiziwa pesa katika akaunti yako. Sehemu fulani ya mapato yako "inazuiliwa" na taasisi ama mtu anaewajibika kukulipa pesa. Mara nyingi kodi hii ni asilimia kumi 10% ya mapato yako. Kama ni gawio, inakatwa 10% ya gawio kabla ya kuingiziwa pesa katika akaunti yako. Hata hivyo, kodi inaweza kuwa chini ya 10% kama tutakavyo ona katika aya zifuatazo.

Umuhimu wa kuzuia kiasi hiki kabla ya kumfikia mwekezaji ni kurahisisha ukusanyaji wa kodi. Kuliko mwekezaji alipe yeye mwenyewe kodi hii, ni rahisi kulipia kupitia kampuni husika inayomlipa mwekezaji. Vinginevyo mapato ya kodi yangeweza kupotea kwa sababu mbalimbali.

Kwa upande wa hatifungani za muda mrefu za serikali, treasury bonds, hakuna makato ya kodi ya zuio. Lakini katika upande wa hatifungani za muda mfupi, yaani treasury bills, kuna makato ya kodi ya zuio ambayo ni 10% ya faida unayostahili. Kwa upande wa hatifungani za kampuni, corporate bonds, kodi ya zuio pia ni 10% ya kiasi unacholipwa kila mwaka, coupon.

Kwa upande wa hisa za makampuni, kodi ya zuio hukatwa wakati wa kulipwa gawio ambapo kodi ya zuio ni 5% ya mapato yako ya gawio. Hakuna kodi ya ongezeko la thamani yaani "capital gain." Hii ina maana kwamba wakati wa kuuza hisa hakuna makato ya kodi hata kama hisa zimepanda thamani kulinganisha na uliponunua. Hata hivyo, hii hutofautiana kati ya nchi moja na nyingine.

Kodi ya zuio kwa makampuni binafsi ni 10% ya mapato. Hapa tunaongelea kampuni zisizoorodheshwa katika soko la hisa DSE. Pia katika makampuni haya kuna makato ya kodi ya ongezeko la thamani ambayo ni 10% ya mapato.

Kwa upande wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja, mutual funds kuna tofauti kadhaa. Mifuko ambayo ni closed-ended inafuata utaratibu wa kawaida wa soko la hisa. Hapa tunaongelea NICOL pamoja na AFRIPRISE. Kwa mifuko hii, kodi ya zuio ni 5% ya gawio. Mifuko ambayo ni open-ended imetofautiana pia. Mifuko yote ya UTT AMIS hakuna makato ya kodi ya zuio. Vilevile Faida Fund ya WHI hakuna makato ya kodi ya zuio.

Mifuko ya Sanlam Investments kuna makato ya kodi ya zuio ambayo ni 10% ya mapato. Wana mifuko miwili ya uwekezaji wa pamoja, na yote ina makato haya. Mfuko wa Timiza wa Zan Securities pia hakuna makato ya kodi ya zuio.

Kipengele kingine ni amana za benki, yaani fixed deposit. Hizi pia huwa na makato ya kodi ya zuio au ongezeko la thamani kutegemea na aina ya akaunti na benki husika. Mara nyingi makato haya yanakuwa ni 10% ya kile kilichoongezeka katika akiba yako.

Mpaka hapo naamini tunao muongozo mzuri kuhusu kodi ya zuio katika uwekezaji wa aina mbalimbali katika masoko ya mitaji na dhamana. Ni vyema kufahamu kuhusu kodi na makato mengineyo ili kuepuka usumbufu. Itasaidia pia kuwa na matarajio yenye uhalisia juu ya tija inayoweza kupatikana katika uwekezaji wako. Kwa sasa tuishie hapo. Tukutane wakati mwingine ili tuendelee kujifunza pamoja. Karibu sana.

Read more