Kuchambua Hati za Muda Mrefu (Security Analysis).
Sasa tupo katika nafasi nzuri kuanza kujifunza mbinu za kuchambua hati za muda mrefu (long-term securities). Tutaanza na upande wa hisa za makampuni (shares).
Security Analysis ni mchakato wa kuchuguza utendaji kazi wa taasisi kabla ya kuamua kununua hati zinazotolewa na hiyo taasisi. Moja kati ya vitu muhimu katika uwekezaji ni kuhakikisha unawekeza katika kitu ambacho unakielewa vizuri, "invest in what you fully understand." Bila kufanya Security Analysis utakuwa bado huna uelewa wa kina juu ya taasisi unayotaka kuwekeza.
Kuna falsafa nyingi sana katika eneo hili la Security Analysis. Ni eneo ambalo wengine wanasomea katika elimu ya juu. Lakini mbinu muhimu za uchambuzi hazihitaji elimu ya chuo kikuu. Tunasema kwamba uchambuzi wa hati sio sayansi ya rocket, "security analysis is not rocket science." Hii ni kama hamasa kwa mtu ambaye hana elimu rasmi (formal education) ya maswala haya. Hesabu kidogo tu za kujumlisha, kutoa, kuzidisha na kugawanya zinatosha kukupatia picha kamili ya utendaji kazi wa taasisi husika. Ni muhimu pia ukajenga tabia ya kufuatilia habari za biashara na kusoma machapisho mbalimbali kuhusu hizo taasisi, kama vile ripoti ya mwaka (annual report).
Kwa ujumla kuna mbinu kuu tatu za Security Analysis: Fundamental Analysis, Technical Analysis na Sentiment Analysis. Katika muktadha wa hati za muda mrefu tutajikita zaidi upande wa Fundamental Analysis.
Fundamental Analysis ni mbinu ya uchambuzi yenye lengo la kuchunguza visababishi vya msingi (fundamentals) vya utendaji kazi wa taasisi husika. Tunaangalia vitu ambavyo vina athari za moja kwa moja katika utendaji kazi, kama vile mfumo wa uongozi (management), ushindani (competition), ukubwa wa soko (market capitalization), nakadhalika. Hapa pia tunapima uwezo wa kampuni kuzalisha faida (profitability), uwezo wa kubana matumizi (cost effectiveness), kiwango cha ukwasi wa kampuni (liquidity), na mengineyo.
Fundamental Analysis inaweza kugawanyika katika makundi mawili ambayo ni Qualitative Analysis na Quantitative Analysis. Qualitative analysis inaonesha mwenendo wa kampuni bila kutumia tarakimu, kwa mfano kuangalia ubora wa mfumo wa uongozi. Quantitative Analysis inaonesha utendaji kazi wa kampuni kwa kutumia tarakimu, kwa mfano uwiano wa faida na mtaji (return on equity/assets). Ni muhimu kufanya uchambuzi wa aina zote mbili ili kupata picha kamili.
Vitu vya muhimu kuzingatia katika Qualitative Analysis ni kama vile;
- Kuwepo au kutokuwepo kwa ushindani (competition vs. monopoly),
- Ukubwa wa soko (market capitalization/size),
- Mfumo wa uongozi (management),
- Mbinu za kumfanya mteja anunue huduma au bidhaa zaidi (lock-in strategies),
- Mbinu za kujitangaza (marketing),
- Ubora wa huduma kwa wateja (customer service),
- Aina ya bidhaa au huduma (which sector?),
- Maoni ya watu kuhusu huduma au bidhaa (customer reviews),
- Ubunifu (innovativeness),
- Uhitaji wa bidhaa au huduma (market demand), nakadhalika.
Vitu muhimu vya kuangalia katika Quantitative Analysis havipo wazi kwa watu wengi, kutokana na kuhusisha tarakimu. Hata hivyo, huwezi kutegemea Qualitative Analysis pekee. Muonekano wa nje hautoshi!
Vitu muhimu katika Quantitative Analysis ni kama vile;
- Bei ya hisa (share price, P),
- Idadi ya hisa zilizotolewa na taasisi (number of issued shares, N),
- Faida baada ya makato (net profit, PAT),
- Mtaji wa wanahisa (total shareholders' equity, E),
- Gawio kwa hisa moja (dividend per share, D),
- Faida kwa hisa moja (earnings per share, EPS),
- Thamani ya hisa (book value, V),
- Ukwasi wa kampuni (net cashflow, C),
- Uwiano wa faida na mtaji wa wanahisa (return on equity, ROE),
- Uwiano wa gawio na bei ya hisa (dividend yield, DY),
- Uwiano wa bei na faida ya hisa moja (price to earnings ratio, PER),
- Uwiano wa bei na thamani ya hisa moja (price to book value ratio, PVR),
- Uwiano wa gharama na kipato (cost to income ratio, CTI),
- Asilimia ya mikopo chechefu (non-performing loans, NPL),
- Uwiano wa faida na mali zote (return on assets, ROA), nk.
Kama unavyoweza kuona hapo juu, Quantitative Analysis inaonekana kuwa na mambo mengi! Hata hivyo, tutajikita kuangalia baadhi ya viashiria, ambavyo ni muhimu zaidi. Kwa leo tuishie hapo.