Mapato Katika Uwekezaji.

Mapato Katika Uwekezaji.
Mapato Katika Uwekezaji

Karibu tena katika blog yetu. Tunaendelea kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji, na siku ya leo tutaangalia aina za mapato yanayoweza kupatikana katika uwekezaji.

Kuna aina kuu mbili za mapato katika uwekezaji, ambazo ni riba (interest) pamoja na faida (profit). Tutaangalia aina zote mbili ili kupata ufahamu zaidi wa nini cha kutarajia kutokana na uwekezaji unaofanywa.

Tuanze na dhana ya riba (interest). Kiufupi riba ni malipo anayopata mwekezaji kwa kuamua kuahirisha kutumia pesa katika matumizi mengine. Ni malipo anayopata kwa sababu pesa taslimu zina thamani kubwa zaidi hivi sasa kulingana na wakati ujao. Binadamu tuna asili ya kuthamini zaidi pesa zilizopo sasa kuliko pesa tunazoweza kupata wakati ujao.

Unapoamua kukopesha pesa unastahili kulipwa riba kwa sababu ungeweza kutumia pesa hizo hivi sasa badala ya kuahirisha kutumia. Kufikia wakati wa kulipwa pesa zako, hazitakuwa na thamani kubwa kulinganisha na zilivyo kwa sasa. Hiyo ndiyo sababu ya kulipwa riba. Vilevile, unapoamua kukopa pesa benki, unawajibika kuwalipa riba kwa sababu hiyohiyo.

Mfano wa uwekezaji ambapo mapato ya riba hupatikana ni katika hatifungani za muda mrefu (bonds). Kila mwaka unalipwa kiasi maalumu cha riba kama tija kutokana na uwekezaji wako. Baada ya muda wa ukomo kutimia utalipwa kiasi cha mwanzo ulichotoa kuikopesha hiyo taasisi. Ni wazi kwamba mpaka kufikia wakati huo hizo pesa zitakuwa zimepungua thamani kulinganisha na hivi sasa. Riba unayolipwa ni kwa ajili hiyo.

Sasa tugeukie upande wa faida (profit). Kiufupi faida ni malipo anayopata mwekezaji kwa sababu ya kuhatarisha (taking risk) mtaji wake. Kutokana na hali ya hatari (risk) iliyopo katika aina mbalimbali za uwekezaji, kigezo kikubwa cha kufanya uwekezaji huo ni kupata faida baadae. Faida ni kama zawadi unayopata kutokana na uthubutu wako. Hata hivyo, kupata faida sio matokeo pekee ya uwekezaji. Unaweza kupata hasara pia.

Mwekezaji anayetaka kupata faida hutumia muda kufanya uchunguzi kabla ya kuwekeza. Lengo ni kutaka kuona kiwango cha hatari pamoja na faida inayoweza kupatikana katika uwekezaji husika.

Mapato aina ya faida hupatikana katika uwekezaji kama vile kumiliki hisa, kumiliki nyumba ya kupangisha, nakadhalika. Tofauti na ilivyo kwa upande wa riba, mara nyingi ni ngumu kukadiria kiwango cha faida inayoweza kupatikana katika uwekezaji. Mtu mwenye bonds ana uhakika wa kulipwa kiasi maalumu kila mwaka. Mtu mwenye hisa hana uhakika huo.

Sasa tuangalie kwa undani zaidi kuhusu mapato ya uwekezaji katika hisa. Faida unayopata kwa kumiliki hisa ni ya namna mbili. Faida ya kwanza ni kuongezeka kwa thamani ya mapato ya kila hisa moja (earnings per share (EPS)) na nyingine ni gawio (dividend). Hivi vitu viwili ndio huunda faida katika kumiliki hisa.

Chukulia mfano EPS ilikuwa ni TZS. 350 wakati wa kununua hisa tarehe 1 Januari 2024. Ilipofika tarehe 30 Juni 2024 ukalipwa gawio la TZS. 40 kwa kila hisa moja. Ilipofika tarehe 31 Julai 2024 EPS ikafika TZS. 500 na ukaamua kuuza hisa zako. Jumla ya faida hapa ni TZS. 190 kwa hisa moja, ambapo TZS. 150 ni kutokana na kuongezeka kwa EPS na TZS. 40 ni kutokana na gawio. Faida hii ingeweza kuwa kubwa au ndogo zaidi kutokana na hatari katika uwekezaji.

Lakini kitu kingine katika mfano wetu hapo juu ni mtazamo wa soko kuhusu hisa husika. Chukulia bei ya hisa tarehe 1 Januari 2024 ilikuwa TZS. 500 ulipokuwa unanunua, na bei ikapanda hadi TZS. 1000 ilipofika tarehe 31 Julai 2024. Hapa kuna ongezeko la TZS. 500 ambalo ni kutokana na mwitikio wa soko kwa ujumla. Kiwango hiki kitaongeza mapato katika uwekezaji wako, lakini hakiangaliwi kama mapato ya uwekezaji, bali mapato ya kubashiri (speculative return). Wewe binafsi hauna uwezo wa kutabiri kwamba bei ya hisa itapanda ama itashuka, na kufanya hivyo ni kubashiri (speculation) sio kuwekeza (investment).

Kwa kuwa bei ya hisa imepanda, utapata jumla ya mapato ya TZS. 690 kwa kila hisa moja wakati wa kuuza hisa zako. Baada ya kukokotoa asilimia tunaona mapato ya uwekezaji (investment return) ni 54.3% na mapato ya kubashiri (speculative return) ni 100%.

Kitu cha msingi katika uwekezaji wa hisa ni kwamba thamani (value) huvuta pesa. Kama hisa za kampuni fulani zinazalisha mapato makubwa ya EPS pamoja na gawio kubwa, bei ya hisa hizo itapanda. Hii ni kwa sababu soko kwa ujumla huwa na matamanio (greed) ya kunufaika kutokana na hisa hizo. Hii hupelekea bei ya hisa hizo kupanda.

Nadhani mpaka sasa tunao uelewa mzuri zaidi juu ya mapato katika uwekezaji. Ni muhimu kukumbuka kwamba kuna athari ya mfumuko wa bei (inflation) ambayo hupunguza sehemu ya mapato hayo. Inflation ina athari katika mapato ya aina zote mbili, haijalishi ni riba au faida.

Mpaka hapo hatuna la ziada katika andiko hili. Tutakutana wakati mwingine ili tuzidi kujifunza kuhusu uwekezaji. Swali la leo kwako msomaji ni: Kuna tofauti gani kati ya kuwekeza (investment) na kubashiri (speculation)?

Read more