Mfuko wa Ukwasi (UTT Liquid Fund).

Mfuko wa Ukwasi (UTT Liquid Fund).

Siku ya leo tutaangalia dondoo chache kuhusu mfuko wa ukwasi uliopo chini ya usimamizi wa UTT AMIS.

Ni mfuko maarufu miongoni mwa wawekezaji hapa Tanzania, lakini bado kuna watu hawajui kiundani kuhusu mfuko huu. Ni mfuko wenye thamani kubwa zaidi ya mifuko yote ya uwekezaji wa pamoja hapa nchini. Hivi karibuni thamani ya mfuko huu ilivuka shilingi trilioni mbili za kitanzania.

Mfuko wa ukwasi ni open-ended mutual fund kwa maana ya kwamba hakuna idadi maalumu ya vipande. Kuelewa zaidi dhana hii unaweza kusoma pia blog hii hapa: https://blog.fintantech.com/mifuko-ya-uwekezaji-wa-pamoja-collective-investment-schemes-2/

Sambamba na kuwa open-ended, mfuko wa ukwasi ni kwa ajili ya kukuza mtaji (growth scheme). Hii ina maana kwamba thamani ya uwekezaji wako itakuwa inaongezeka lakini hakuna tija nyingine tofauti na hiyo. Hakuna gawio bali ukuaji wa mtaji pekee. Hii ni sababu kubwa katika kupelekea thamani ya mfuko huu kuongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi ya mifuko mingine.

Mfuko wa ukwasi ulianzishwa rasmi mwaka 2013 ambapo bei ya awali (issue price) ilikuwa TZS. 100 kwa kipande kimoja. Bei ya sasa ni TZS. 413.35 kwa kipande kimoja. Hili ni ongezeko la 313.35% katika thamani ya kipande.

Kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 100,000 na unaweza kuongeza uwekezaji kwa kuanzia na TZS. 10,000 tu. Hakuna kiwango cha mwisho cha uwekezaji. Unanunua vipande moja kwa moja kutoka kwa wasimamizi wa mfuko, sio kupitia soko kama DSE. Bei ya kipande kimoja ni sawa kabisa na thamani ya kipande. Sio kama ilivyo kwa upande wa hisa.

Sera ya uwekezaji (investment policy) ya mfuko huu ni kuwekeza 100% ya mtaji katika soko la fedha (money market) pamoja na hatifungani za muda mrefu (bonds). Tafsiri yake ni kwamba kuna hatari ndogo (low risk) katika uwekezaji huu. Hii inapelekea mfuko kuwa na sifa ya ukwasi mkubwa pamoja na hatari ndogo.

Kingine ni kwamba hakuna makato ya kununua au kuuza vipande vya mfuko huu. Unanunua au kuuza kwa bei ya wakati huo bila kuwa na makato. Kama unataka kuwekeza TZS. 100,000 basi kiasi chote kitatumika kununua vipande. Vilevile kama unataka kuuza vipande vyenye thamani ya laki moja, laki moja yote itaingia kwenye akaunti yako.

Unaweza kununua vipande kwa njia kadhaa ikiwemo kutumia njia ya benki kama CRDB, Stanbic, nk. Unaweza kuuza vipande kwa kutumia menyu yao ya simu ya mkononi, au kwa kutumia app.

Kabla ya kuamua kununua vipande ni vizuri uwe na mkakati wa kuwekeza. Ni vizuri pia ufanye uchambuzi wa mfuko husika. Pitia ripoti za kifedha za mfuko. Soma waraka wa matarajio wa mfuko.

Ripoti za kifedha zitakupa mwanga juu ya utendaji kazi wa mfuko. Zitasaidia kuelewa mfuko unazalisha pesa kutokana na vyanzo gani na kwa kiwango gani. Kwa mfano, ripoti (balance sheet) ya miezi sita kufikia tarehe 31 Disemba 2023 inaonesha mfuko unamiliki TZS. 856,415.683 million kutokana na hatifungani za serikali (treasury bonds) ambayo ni 95.4% ya mali zote kwa kipindi husika. Hii inakupa picha kwamba uwekezaji huu ni salama kama wanavyoahidi katika sera ya uwekezaji.

Hizo ni baadhi ya dondoo muhimu juu ya mfuko wa ukwasi. Mara nyingi watu wanawekeza katika mfuko huu kwa malengo ya kuweka akiba na sio kutengeneza utajiri. Ni sehemu salama kwa kuweka akiba lakini huwezi kuzalisha faida kubwa kwa kupitia mfuko huu.

Hapo tumefikia tamati ya andiko hili la leo. Ni vyema kujipa muda wa kufuatilia zaidi kuhusu mfuko huu na mingineyo. Elimu ni silaha muhimu sana katika uwekezaji wako. Tutakutana wakati mwingine ili tuendelee kujifunza pamoja. Nakutakia heri katika uwekezaji wako.

Read more