Mfumo wa Fedha (Financial System).

Mfumo wa Fedha (Financial System).
MFUMO WA FEDHA

Mfumo wa fedha ni namna maalumu ya kuwaunganisha watu wenye ziada za mitaji (excess funds) pamoja na watu wenye uhitaji wa mitaji. Bila kuwa na namna maalumu ya kuwaunganisha watu hawa, inakuwa ngumu kwa watu kufanya baadhi ya biashara ama manunuzi. Mfano ni inapotokea mtu anahitaji kununua nyumba lakini hana akiba ya kutosha kufanya hivyo. Mfumo wa fedha kupitia benki utamsaidia mtu huyo kupewa mkopo kwa ajili ya kununua gari, endapo atakidhi vigezo. Mfano mwingine: Mtu ana wazo zuri la biashara lakini hana mtaji. Mtu huyu anaweza kuomba mkopo wa biashara kupitia benki. Namna nyingine ni kujiorodhesha katika soko la hisa na kuuza sehemu ya umiliki wa mali na faida itakayopatikana kupitia kampuni hiyo.

Mfumo wa fedha ni mhimili muhimu sana katika kuimarisha uchumi wa nchi. Kukiwa na dosari katika mfumo huu, mazingira ya kufanya biashara huwa magumu sana, kama ilivyo kwa nchi nyingi zinazoendelea (developing countries). Sambamba na hilo, mfumo wa imara wa fedha unasaidia kutoa fursa kwa watu binafsi kufanya uwekezaji katika uchumi wa nchi yao. Mfumo wa fedha ukiwa imara, mzunguko wa fedha kati ya watu unakuwa rahisi, na inasaidia kupunguza uhalifu.

Mfumo wa fedha unaundwa na taasisi za kifedha (financial institutions) kama benki, mifuko ya uwekezaji wa pamoja (mutual funds), soko la mitaji (capital market), soko la fedha (money market), mifuko ya pensheni (pension funds), mifuko ya bima (insurance funds), nakadhalika. Benki kuu (central bank) pamoja na benki za biashara (commercial banks) ni sehemu muhimu sana katika mfumo wa fedha. Mfumo wa fedha upo chini ya usimamizi mkali kuliko sekta ama mifumo mingine yoyote ya uchumi katika nchi husika.

Jitihada nyingi zinafanyika ili kuweza kuongeza ushiriki wa watu katika mfumo wa fedha (financial inclusion). Asilimia kubwa ya watanzania bado hawana akaunti benki, na wengi wao wanaweka akiba kwa njia zisizo salama. Asilimia ndogo sana ya watanzania ndio wana uelewa kuhusu fursa za kuwekeza kupitia mfumo wa fedha. Wengi wanasikia kuhusu "hisa," "hatifungani," "vipande," "gawio," na misamiati mingine ya kifedha (financial jargon), lakini bado wana uelewa mdogo.

Kupitia blog hii utapata uelewa wa kina zaidi kuhusu mfumo wa fedha, na elimu yako itakuwa ukombozi wako.

Read more