Mtazamo wa Uwekezaji (Investment Mindset).
Ni wakati mwingine tena nimepata nafasi ya kuandika maandishi. Karibu sana katika pango la maarifa, tujifunze pamoja. Siku ya leo tutaangalia mtazamo wa uwekezaji, na tutaona ni jinsi gani kuwa ama kutokuwa na mtazamo wa uwekezaji kunaweza kubadilisha maisha yako.
Uwekezaji ni mchakato wa kununua mali inayoongezeka thamani kadri muda unavyoenda. Hapa mtu anajaribu kutafuta mali ambayo akiinunua kwa mtaji alionao (capital), basi ataweza kunufaika aidha kupitia ongezeko la thamani (capital gain), kupata gawio (dividend), kulipwa kipato maalumu (fixed income), nakadhalika. Uwekezaji wenye tija ni "mchakato," sio kitu cha kukurupuka.
Mwekezaji makini (Intelligent Investor) ana sifa nyingi muhimu. Sifa yake kubwa ni uwezo wa kudhibiti tabia yake wakati wa kufanya maamuzi ya kununua na kuuza mali. Ukweli ni kwamba hakuna mtu mwenye uwezo wa kudhibiti mwenendo wa bei katika masoko ya mitaji. Kitu pekee unachoweza kufanya ni kudhibiti tabia yako ili isiwe kikwazo katika uwekezaji. Tunaposema kudhibiti tabia tuna maana ya kwamba ili uwe mwekezaji makini, ni muhimu kufanya maamuzi kwa utulivu, bila kuendeshwa na hisia (sentiment/emotions).
Unamkuta mtu ananunua hisa za CRDB kwa sababu ni benki anayoipenda. Huu sio mtazamo wa uwekezaji, bali kuruhusu hisia zako ziingilie maamuzi yako ya kuwekeza. Anakwambia CRDB ni benki inayofanya vizuri sana, lakini hana uthibitisho wowote wa madai kama hayo. Kama unaamua kununua mali unayoamini itapanda thamani, lazima imani yako iwe na msingi.
Kununua hisa bila kufanya uchambuzi wa kampuni ni sawa na kucheza kamali (gambling). Unachezea pesa zako, na una uwezekano mkubwa wa kuzipoteza. Hata inapotokea umefanikiwa kupata faida, bado hautakuwa na uwezo wa kupata faida endelevu. Kinachokuja kiurahisi huondoka kiurahisi pia. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, kama umejibana na kuweka akiba kwa nidhamu, kwanini unachezea pesa zako?
Mwekezaji makini ni mtu mwenye malengo ya muda mrefu. Uzoefu unaonesha kwamba ongezeko la thamani ya mali huchukua muda mpaka kuweza kuona tija yoyote. Mara nyingi inamlazimu mwekezaji kusubiri miaka kadhaa kabla ya kuanza kufaidika na uwekezaji wake. Fikiria miaka mitano na kuendelea, kisha weka malengo thabiti ya uwekezaji. Hakuna njia fupi (shortcut) ya kuufikia uhuru wa kifedha (financial freedom). Kwa kutumia kanuni ya riba ambatani (compound interest) na kuwekeza mara kwa mara (annuity), unaweza kupiga hatua kubwa. Kitu cha msingi ni muda. Ni vizuri kuanza mapema iwezekanavyo ili uweze kuona maajabu ya kanuni hizi rahisi za uwekezaji.
Mwekezaji makini anatumia muda mwingi kufanya uchambuzi (analysis) kabla ya kuwekeza, lakini baada ya hapo kazi yake inakuwa imeisha. Unatumia nguvu kubwa mwanzoni, kisha unaisubiri nguvu ya muda (time) na bahati (chance). Bahati inahusika pia, lakini kila mmoja kwa kiwango chake. Cha msingi ni kwamba lazima uweke jitihada binafsi, na sio kutegemea bahati (chance). Unaweka jitihada katika kufuatilia utendaji kazi wa makampuni, taarifa muhimu za biashara, sera za nchi, nk. Fuatilia kuhusu mali kabla ya kuimiliki.
Mwekezaji makini ananunua mali (assets) na sio wajibu (liabilities). Hii haina maana kwamba kila kitu unachomiliki kinaongezeka thamani. Hapa tunaangalia mtu anapokuwa anataka kuwekeza. Kama unataka kuwekeza, nunua mali inayopanda thamani, na sio kitu kinachoshuka thamani au kuongeza gharama za maisha. Kama unataka gari liwe mali, lifanye hilo gari kuwa gari la abiria au mizigo na sio la kusafiria wewe mwenyewe. Kama unataka nyumba iwe mali, weka wapangaji na sio kuishi wewe mwenyewe. Kama unataka simu yako iwe mali, itumie kuingiza pesa mtandaoni au kuongeza wateja wa biashara yako, nk.
Mwekezaji makini sio lazima awe mfanyabiashara. Biashara sio kwa ajili ya kila mtu. Lakini mtu yeyote anaweza kuwekeza, hata kama ni mwajiriwa. Kama unatamani kutengeneza ukwasi, fikiria njia zaidi za kuingiza pesa hata ukiwa usingizini. Kama unamiliki biashara na inakuhitaji uwepo ili mambo yaende, hapo bado haujaweza kuifanya biashara yako kuwa uwekezaji/mali. Kama umeajiriwa fikiria jinsi unavyoweza kuanza kuwekeza, kwa mfano katika soko la mitaji (capital market). Ukiwa na malengo thabiti, haijalishi umeajiriwa ama umeajiri watu wengine. Wote wanaweza kufikia uhuru wa kifedha (financial freedom).
Uvumilivu ni sifa muhimu sana ya mwekezaji makini. Dhibiti hisia zako. Jipe muda wa kutosha. Fuatilia kuhusu uwekezaji kwa njia mbalimbali kama kusoma vitabu, kusikiliza ushauri wa wataalamu, nk. Ni imani yangu kwamba jitihada hizi zinaweza kutusogeza mbali na ukata na kutuweka pembezoni mwa ukwasi. Tukutane tena wakati mwingine ili tuendelee kujinoa katika uwekezaji. Swali langu kwako ni kwamba, una mpango wa kustaafu lini? Kama bado hujui jibu la swali hili, hakikisha umepata majibu mapema iwezekanavyo.