Riba Ambatani (Compound Interest).
Karibu tena ndugu msomaji. Karibu tena tujifunze pamoja. Karibu tujifunze kuhusu kanuni ya riba ambatani, ambalo ni "ajabu la nane la dunia." Kanuni hii ni moja kati ya kanuni za msingi zaidi katika kutengeneza kipato tulivu (kuzalisha pesa bila uwepo wako yaani "passive income."). Huenda ni kweli kwamba unaweza kuingiza pesa nyingi ukiwa usingizini kuliko unavyoweza kuzalisha pesa ukiwa macho. Huenda tunatumia nguvu nyingi kwenye mambo madogo ama yasiyohitaji nguvu kiasi hicho.
Msingi wa riba ambatani ni kwamba riba unayolipwa inatengeneza sehemu ya mtaji na hivyo kuzalisha riba kubwa zaidi baadaye. Hapa tunaongelea kuwekeza faida unayopata ili kuzalisha faida kubwa zaidi. Tunaanza na riba ya mwanzoni kabisa, kisha tunapata mlolongo mrefu wa riba hapo baadae. Ukilipwa gawio unatumia pesa za gawio kununua hisa zaidi. Hisa hizo pia zitaleta gawio baadae, ambalo utanunulia tena hisa, nk.
Kama mtaji uliowekezwa awali utabakia vilevile bila jitihada za kuwekeza faida unayopata, thamani ya uwekezaji wako itapungua. Kama unataka kutengeneza utajiri, usiwaze kutumia faida unayopata kwa ajili ya matumizi binafsi. Angalia namna nyingine za kukidhi mahitaji huku ukilenga kuongeza thamani ya uwekezaji wako ambayo ndiyo picha halisi ya utajiri wako.
Katika mlolongo huu wa riba ambatani, anayeanza mapema ndiye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kutengeneza utajiri. Muda sahihi zaidi wa kupanda miti ulikuwa miaka ishirini iliyopita. Muda mwingine sahihi wa kupanda miti ni sasa. Kadri unavyoanza mapema, ndivyo unavyojitengenezea nafasi kubwa zaidi ya kuzalisha faida kubwa baadae.
Kitu cha msingi ni kuhakikisha kwamba unaendelea kuishi ndani ya bajeti yako hata kama kipato chako kimeongezeka kiasi fulani. Lenga zaidi kukuza thamani ya uwekezaji wako, sio matumizi. Kama matumizi yako yameongezeka kutokana na kuwa na kipato kikubwa zaidi, thamani ya uwekezaji wako haitaweza kuongezeka kwa sababu "umekula faida."
Ili uweze kufaidika kutokana na kanuni ya riba ambatani, ni muhimu uwe na chanzo cha kipato cha kutosheleza mahitaji ya kila siku. Vinginevyo utaanza kutumia pesa unazopata kama faida kutokana na uwekezaji wako. Kufanya hivyo ni kudumaza uwekezaji wako. Ndio maana ni muhimu kuwa na kazi ya kuingiza kipato wakati unafanya uwekezaji. Usitegemee kwamba uwekezaji wako ni kwa ajili ya matumizi binafsi. Uwekezaji ni kwa ajili ya mahitaji ya baadae, kipindi ambacho hautakuwa na uwezo wa kufanya tena kazi aidha kwa lazima ama kwa hiari yako. Ndio maana tunasema ni muhimu kujua mapema kuhusu kustaafu kisha kuweka malengo thabiti ya uwekezaji.
Kanuni hii ya riba ambatani itasaidia kukuza thamani ya uwekezaji wako kipindi ambacho wewe upo unaendelea kufanya kazi. Ndio maana tunasema riba ambatani inazalisha kipato tulivu. Endapo mtaji unaongezeka thamani kadri muda unavyokwenda, hata riba unayopata itaongezeka zaidi na zaidi, bila hata kuhitaji uwepo wako. Cha msingi ni kuwa na nidhamu ya kubana matumizi, na kuwa na subira.
Riba ambatani inaweza kuzalisha faida kubwa baada ya muda. Inaweza kufanya thamani ya uwekezaji wako ikue zaidi na zaidi. Kanuni hii ni ya msingi sana katika kuongeza thamani ya uwekezaji. Vinginevyo utafanya kazi miaka mingi na kuendelea kutokuwa na uhuru wa kifedha. Sio ajabu kuona watu wengi wanaendelea kuteseka katika "mashindano ya panya."
Watu wengi wanaweza kuingiza pesa, lakini hawawezi kutengeneza utajiri. Tumia kanuni ya riba ambatani ili kutengeneza utajiri. Fanya kazi kwa bidii, bana matumizi, weka akiba, wekeza akiba yako, wekeza faida unayopata kutokana na uwekezaji wa awali. Jipe muda wa miaka kadhaa kwa ajili ya kutekeleza mpango huu, kisha acha maajabu ya muda na bahati yafanyike.
Naomba tuishie hapo ndugu msomaji. Tukutane tena wakati mwingine ili tuendelee kujifunza uwekezaji. Kutengeneza utajiri ni mchakato. Tutaendelea kujifunza pamoja jinsi ya kutengeneza utajiri kupitia uwekezaji.