Security Analysis Pt. 2

Security Analysis Pt. 2
Security Analysis

Karibu tena tuendelee na somo la Security Analysis kwa upande wa hisa (shares). Qualitative analysis haina changamoto kubwa, lakini kuna mambo kadhaa ya kuzingatia. Kuna sekta zinafanya vizuri zaidi kuliko nyingine, hivyo ni muhimu kuwekeza katika sekta hizo. Mfano wa sekta zinazofanya vizuri Tanzania ni sekta ya fedha na uwekezaji (finance and investment) pamoja na sekta ya viwanda (manufacturing). Hapa tunaongelea kampuni kama vile NMB, CRDB, DSE, NICOL, AFRIPRISE (mwanzoni iliitwa TICL), TWIGA CEMENT (TPCC), nakadhalika. Finance and investment ni sekta inayoongoza kwa kutengeneza utajiri mkubwa duniani, na matajiri wengi wamewekeza katika sekta hiyo.

Jambo lingine muhimu kuzingatia katika Qualitative Analysis ni kuwepo au kutokuwepo kwa ushindani. Kampuni kama vile DSE haina ushindani ndani ya nchi ya Tanzania (monopoly), kwa sababu ndilo soko pekee la hisa (stock exchange). Upande wa benki pia NMB na CRDB ni benki zenye wateja wengi zaidi kwa Tanzania. Nchi ya Tanzania bado hakuna ushindani mkubwa katika baadhi ya sekta, na hiyo ni fursa kwa wawekezaji.

Kitu kingine cha kujiuliza ni kama hiyo kampuni inafuata taratibu na sheria za nchi kama zinavyosimamiwa na taasisi kama CMSA, DSE, BRELA, TRA, BOT, nk. Mara kadhaa kampuni zinaondolewa katika soko la hisa la DSE kutokana na kushindwa kukidhi baadhi ya masharti. Kampuni nyingine wanaweza kutoa taarifa kwa umma na kuahidi kutoa faida na gawio kubwa lakini ni muhimu kuwa makini sana. Ni rahisi sana kutapeliwa katika mambo haya ya uwekezaji katika sekta ya fedha na uwekezaji.

Sasa tuhamie upande wa Quantitative Analysis tuangazie jinsi ya kukokotoa baadhi ya viashiria muhimu vya utendaji (Key Performance Indicators, KPIs).

  1. RETURN ON EQUITY (ROE): Hiki ni kiashiria cha uwiano kati ya faida baada ya makato (PAT) na mtaji wa wanahisa (shareholders' equity, E). Baada ya kupata thamani ya ROE tunalinganisha na riba ya hatifungani ya miaka kumi ambayo ni kama wastani (benchmark). Kulingana na riba mpya (new coupon rates), riba ya hatifungani ya miaka kumi ni 10.25%. Kama ROE ipo chini ya hapo inaashiria utendaji wa chini ya kiwango. Ili kupata thamani ya ROE tunahitaji kutumia INCOME STATEMENT kuangalia faida baada ya makato, na BALANCE SHEET kuangalia mtaji wa wanahisa. Mfano ni kampuni ya CRDB ambapo kulingana na ripoti ya mwaka 2023, thamani ya faida baada ya makato (PAT) ni TZS. 422.792 billion na mtaji wa wanahisa (shareholders' equity, E) ni TZS. 1,737.876 billion. Tukigawanya hizi namba mbili tunapata ROE ni 24.3%.
  2. PRICE TO EARNINGS RATIO (PER): Hiki ni kiashiria cha uwiano kati ya bei ya hisa moja (share price, P) na faida kwa hisa moja (earnings per share, EPS). PER chini ya 5 inaashiria hisa ina bei ndogo sana (very cheap). PER kati ya 5 na 20 inaashiria bei ni nafuu (affordable). PER zaidi ya 20 inaashiria bei ni ghali (expensive). Bei ya hisa moja ya CRBD ilikuwa TZS. 460 kwa tarehe 31 Desemba 2023. Faida kwa hisa moja inapatikana kwa kugawanya faida baada ya makato (PAT) kwa idadi ya hisa (total issued shares, N). Kulingana na Income Statement, PAT ni TZS. 422.792 billion. Idadi ya hisa, N ni 2,611,838,584 kulingana na ripoti ya mwaka 2023 ya CRDB. Baada ya kugawanya tunapata EPS ni TZS. 161.9, ambayo tunatumia kutafuta PER. Tukigawanya bei ya hisa kwa EPS tunapata PER ni 2.8.
  3. PRICE TO VALUE RATIO (PVR): Hiki ni kiashiria cha uwiano kati ya bei ya hisa, P na thamani ya hisa, V. Thamani ya hisa moja inapatikana kwa kugawanya mtaji wa wanahisa (shareholders' equity, E) kwa idadi ya hisa, N. Endapo thamani ya hisa ni kubwa kuliko bei ya hisa tunapata PVR chini ya 1. Endapo PVR ni zaidi ya 1 inaashiria bei ya hisa ni kubwa kuliko thamani ya hisa. Kulingana na Balance Sheet ya CRDB ya tarehe 31 Desemba 2023, mtaji wa wanahisa, E ni TZS. 1,737.876 billion. Idadi ya hisa, N ni 2,611,838,584. Tukigawanya tunapata thamani ya hisa, V ni TZS. 665.4 kwa hisa moja. Tukigawanya bei TZS. 460 kwa thamani TZS. 665.4 tunapata PVR ina thamani ya 0.69.

Kwa machache tuliyojifunza inatosha tukaishia hapo kwa sasa. Tutaendelea na uchambuzi huu mpaka tupate uelewa mzuri. Jipe muda kupitia vizuri mahesabu ya ROE, PER na PVR. Pakua ripoti ya CRDB ya mwaka 2023 kupitia link hii: https://crdbbank.co.tz/storage/app/media/2023%20CRDB%20BANK%20ANNUAL%20REPORT.pdf

Read more