Security Analysis Pt. 3
Karibu tena tujifunze Security Analysis. Tunaendelea na kipengele cha Quantitative Analysis tulipoishia. Kama ni mara yako ya kwanza kusoma blog hii ni vyema ukapitia post iliyopita kwanza. Tunaendelea na Key Performance Indicator (KPI) namba nne:
- DIVIDEND YIELD (DY): Huu ni uwiano kati ya gawio (dividend per share, D) kwa hisa moja na bei ya hisa moja (share price, P). Kwa kuendelea na mfano wetu wa kampuni ya CRDB, gawio kwa hisa moja kwa mwaka 2023/2024 ni TZS. 50 na bei ya hisa moja kwa tarehe 31 Desemba 2023 ni TZS. 460. Tukigawanya tunapata DY ina thamani ya 10.9%. DY inatumika kulinganisha baina ya kampuni zinazotoa gawio. Thamani kubwa ya DY ni bora zaidi, na inaonesha kampuni sahihi zaidi ya kuwekeza. Hata hivyo, kuna kampuni hazitoi gawio na zinafanya vizuri. Ni vyema kutumia kigezo cha DY pamoja na vigezo vingine kwa matokeo mazuri zaidi.
- NON-PERFORMING LOANS (NPL): Hii ni mikopo chechefu, yaani mikopo isiyoingiza kipato. Kiashiria hiki kinatumika wakati wa kuchambua utendaji kazi wa benki. NPL inaonesha mikopo chechefu ni asilimia ngapi ya mikopo yote iliyotolewa na benki. Kulingana na masharti ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inatakiwa NPL iwe 5% au chini ya hapo ili benki iwe na idhini ya kutoa gawio kwa wanahisa. Mara nyingi thamani ya NPL inaonekana kwenye kurasa za mwanzoni za ripoti ya mwaka, hivyo hakuna haja ya kukokotoa. Ukurasa wa 18 wa ripoti ya mwaka 2023 ya CRDB una taarifa ya NPL ambayo ni 2.8%.
- COST TO INCOME RATIO (CTI): Huu ni uwiano kati ya gharama za uendeshaji (costs) na mapato ya kampuni (income). Inaashiria gharama ambayo kampuni inatumia ili kutengeneza faida. Kipimo hiki kinafaa katika kupima uwezo wa kampuni kubana matumizi (cost effectiveness). Mara nyingi tunatumia CTI katika kuchambua utendaji kazi wa benki. Kulingana na maelekezo ya BOT, inatakiwa CTI iwe 55% au chini ya hapo ili benki iwe na idhini ya kutoa gawio kwa wanahisa. Mara nyingi CTI inaandikwa katika kurasa za mwanzoni za ripoti ya mwaka ya benki husika. Ukurasa wa 18 wa ripoti ya mwaka 2023 ya CRDB una taarifa ya CTI ambayo ni 49.5%.
Viashiria hivyo tulivyojadili vikitumika pamoja vinatosha katika kupata picha ya utendaji wa kampuni. Viashiria hivyo ni: ROE, PER, PVR, DY, NPL na CTI. Ni muhimu sana kuangalia vipimo hivi vya uwiano (financial ratios) kuliko kuangalia tarakimu halisi (actual figures) za faida, gawio, bei, nk. Hisa inaweza kuwa na bei kubwa lakini PER yake ipo chini ya 5, ambayo inamaanisha bei ni ndogo sana.
Vilevile ni muhimu kuzingatia kwamba hata kama kampuni inatengeneza faida haina maana kuwa itafanya vizuri katika soko la hisa. Mwenendo wa bei katika soko la hisa unatokana na washiriki katika soko na unaweza kutoa picha tofauti na uhalisia wa kampuni. Unashauriwa kununua hisa kama unavyonunua mahitaji muhimu, sio kama unavyonunua manukato. Uwekezaji unahitaji utulivu wa akili. Haina maana yoyote kuteseka kutafuta pesa na kuweka akiba endapo utapoteza pesa zote katika uwekezaji.
Baada ya kujifunza mambo hayo machache kuhusu uchambuzi wa kampuni, ni vyema tuyafanyie kazi. Tafuta ripoti za makampuni, fanya mazoezi ya kuchambua. Usisubiri upate pesa ndipo ujifunze uchambuzi wa kampuni. Badili mtazamo kuhusu uwekezaji, na utaweza kufika mbali.