Short-term Securities Pt. 2
Karibu tena tuendelee tulipoishia. Baada ya kuangalia kwa ufupi kuhusu treasury bills, sasa tugeukie upande wa amana za muda maalumu za benki (fixed deposit).
Amana ya benki ni hati inayomuwezesha mwekezaji kuweka akiba kwa riba maalumu kwa kipindi fulani, kama vile miezi mitatu, miezi sita na kuendelea. Mwekezaji ana uwezo wa kuongea na watu wa benki husika ili kupewa riba yenye tija zaidi. Hii tunaita "negotiable interest rate." Mara nyingi riba unayolipwa itatosha kukabiliana na mfumuko wa bei, na hakuna makato yoyote kwa kipindi chote cha mkataba.
Hata hivyo, ikitokea unahitaji pesa zako kabla ya muda wa ukomo, kuna uwezekano wa kupoteza mpaka 50% ya pesa. Haya yote unaambiwa wakati wa kununua amana za benki. Wakati wa ukomo ukifika, faida unayopata inakatwa 10% kama kodi ya zuio (withholding tax). Haya makato ni kwenye faida tu, sio mtaji uliowekezwa awali.
Mara nyingi riba unayolipwa ni chini ya 1% kwa mwezi. Unaweza kulipwa riba ya 4.5% kwa miezi sita. Viwango vitatofautiana kutoka benki moja kwenda nyingine, kulingana na makubaliano pia.
Mara nyingi kiwango cha chini cha uwekezaji katika amana za benki ni TZS. 500,000. Inawezekana kuwa chini au zaidi ya hapo kulingana na bidhaa maalumu za benki husika. Kitu cha msingi ni kufuatilia benki mbalimbali zinatoa amana za sifa gani.
Faida ya amana za benki ni kwamba unao uwezo wa kutumia kuomba mkopo mpaka 90% ya pesa zako. Amana za benki zinakubalika kiurahisi kwa sababu ni pesa, hivyo ukwasi (liquidity) sio changamoto. Faida nyingine ni usalama wa pesa zako. Sio rahisi kupoteza pesa, labda itokee benki imefilisika.
Hasara ya amana za benki ni kuwa na faida ndogo kulinganisha na aina nyinginezo za uwekezaji. Hata hivyo, faida unayopata inakuwa ya uhakika.
Kabla ya kuamua kuweka pesa zako katika akaunti ya namna hii, ni vyema ukawa na uhakika kwamba hautakuwa na matumizi ya pesa hizo katika kipindi chote cha mkataba. Baadhi ya amana za benki watakupa uhuru wa kurudishiwa pesa zako, lakini mara nyingi kutakuwa na makato (penalty).
Muda wa ukomo wa amana za benki unaweza kuwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini tija inayopatikana inakuwa ndogo kulinganisha na dhamana za muda mrefu. Zipo amana za mwaka mmoja, miaka miwili, nk.
Kulingana na muktadha wa Tanzania, treasury bills na fixed deposit ndio dhamana za muda mfupi zinazotumika zaidi. Amana za makampuni (commercial papers) hutolewa na kampuni inapohitaji kukidhi mahitaji ya muda mfupi ya kifedha. Kuhusu fedha za kigeni (forex) ni kwamba benki kuu pamoja na benki nyingine hushiriki katika biashara ya kubadili pesa kwa lengo la kuimarisha viwango vya ubadilishaji (exchange rates). Watu binafsi pia wanashiriki katika soko la forex, lakini ni asilimia ndogo ya soko zima.
Sifa kubwa ya money market ni muda wa ukomo kuwa mfupi kulinganisha na capital market. Sifa nyingine ni ukwasi. Dhamana za muda mfupi zina urahisi wa kubadilishwa kuwa pesa kulinganisha na dhamana za muda mrefu. Mwekezaji anashauriwa kuwekeza asilimia fulani ya mtaji katika dhamana za muda mfupi.
Mpaka hapo tumefikia mwisho wa utangulizi kuhusu dhamana za muda mfupi. Ni vyema kuendelea kujifunza kupitia vyanzo mbalimbali. Elimu ya uwekezaji ni elimu pana, na kujifunza mara kwa mara ni muhimu. Tukutane wakati ujao ili tuzidi kupata elimu.