Soko la Mitaji (Capital Market).
Baada ya kupata utangulizi mfupi kuhusu mfumo wa fedha kwa ujumla, sasa tunaanza kufafanua sehemu mojawapo muhimu sana katika mfumo wa fedha, soko la mitaji.
Soko la mitaji ni njia ya moja kwa moja ya kuwaunganisha watu wenye mitaji ya ziada na watu wenye uhitaji wa mitaji. Ni njia ya moja kwa moja kwa maana ya kwamba hakuna haja ya kukopa benki, bali mhusika mwenye uhitaji anafanya miamala na watu wenye mitaji moja kwa moja kupitia soko la awali (primary market). Sifa muhimu kuhusu soko la mitaji ni kwamba hati zinazotolewa zinakuwa za muda mrefu (long-term securities). Aliye na uhitaji wa mtaji anatoa hati kwa watu walio na mitaji, kana kwamba anauza hati ili apate mtaji. Mifano ya hati za muda mrefu zinazouzwa kwenye soko la mitaji ni hisa (shares or stocks) na hatifungani za muda mrefu (bonds).
Tunaposema hati za muda mrefu inamaanisha kuanzia mwaka mmoja na zaidi, katika muktadha wa Tanzania. Hati za muda chini ya mwaka mmoja huuzwa kupitia soko la fedha (money market). Hiyo ni mada ya siku nyingine.
Hisa ni hati (security) inayotolewa na kampuni kwenda kwa mtu mwenye mtaji (mwekezaji) kama uthibitisho kwamba mwekezaji anamiliki asilimia fulani ya mali na kipato cha kampuni husika. Hisa ni mali (asset) kwa mwekezaji lakini ni wajibu (liability) kwa kampuni. Katika soko la awali, idadi maalumu ya hisa za kampuni inatolewa kwa umma, mchakato unaoitwa Initial Public Offering (IPO). Mara baada ya mauzo kwenye soko la awali kumalizika, hisa za hiyo kampuni hazipatikani tena katika soko la awali, na huhamia katika soko la pili (secondary market). Kampuni inapata mtaji wakati huo wa IPO. Mauzo yoyote ya hisa kwenye soko la awali ndio mtaji wa kampuni husika. Mauzo yanayotokea katika soko la pili ni baina ya wamiliki wa hisa na wanunuzi wa hisa, bila kuhusisha kampuni husika.
Hatifungani ya muda mrefu (bond) ni hati (security) inayotolewa na kampuni (corporate bond) au serikali (treasury bond) kwenda kwa mwekezaji kama ahadi kuwa mwekezaji atalipwa riba maalumu (fixed interest) kwa miaka kadhaa na baadaye kurejeshewa pesa ya mwanzo (face value) aliyoikopesha hiyo kampuni au serikali. Hati hii inakuwa na muda wa ukomo (maturity) mara nyingi kuanzia miaka miwili mpaka ishirini na tano kwa Tanzania. Ndani ya miaka hiyo yote, mwekezaji ana haki ya kulipwa riba maalumu (fixed interest) kila mwaka, ambapo mara nyingi malipo ni mara mbili kwa mwaka (semi-annually). Hatifungani ni mali (asset) kwa mwekezaji na wajibu (liability) kwa kampuni au serikali. Mmiliki wa hatifungani hana umiliki (ownership) wa mali ama kipato cha taasisi inayotoa hatifungani, bali yeye ni mkopeshaji (creditor).
Bonds pia huuzwa katika soko la awali na baadaye kupitia soko la pili, kama ilivyo kwa upande wa hisa. Soko la pili la hisa na bonds kwa Tanzania linajulikana kama Dar es salaam Stock Exchange (DSE). DSE wanahusika pia na IPO za makampuni.
Tofauti muhimu ya hisa na bonds ni kwamba, mmiliki wa bonds anapewa kipaumbele zaidi kuliko mmiliki wa hisa. Hii ni kwa sababu yeye ni mkopeshaji, ilhali mmiliki wa hisa ni mmiliki wa kampuni. Ikitokea hasara au faida katika kampuni, mmiliki wa bonds hahusiki. Mmiliki wa hisa anapata sehemu ya faida au hasara iliyopatikana kulingana na idadi ya hisa anazomiliki.
Huu ni utangulizi tu kuhusu soko la mitaji. Tutaendelea kujifunza zaidi wakati ujao. Zingatia sana kupata uelewa wa kina kuhusu soko la mitaji kabla ya kuamua kufanya uwekezaji huko.