Swali Muhimu Kila Unaponunua Hisa.

Swali Muhimu Kila Unaponunua Hisa.
Swali Muhimu Kila Unaponunua Hisa

Habari ndugu msomaji. Karibu tena katika blog yetu. Siku ya leo tutaangalia moja kati ya maswali muhimu ya kujiuliza wakati wa kununua hisa.

Swali lenyewe ni: Ikiwa sitapata tena nafasi ya kujua mwenendo wa bei katika soko, nitakuwa na amani kumiliki hisa ninazo nunua?

Kutokana na kawaida ya soko la hisa kuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya kupanda na kushuka bei, ni rahisi sana kusahau maana halisi ya kumiliki hisa. Bei ya hisa katika soko ni kulingana na washiriki wa soko la hisa.

Bei ya hisa ni thamani kulingana na mtazamo wa washiriki katika soko. Wao "wanadhani" kwamba hisa za kampuni X zinafaa kuuzwa kwa bei fulani, hivyo tunaiita thamani kimtazamo (Perceived Value).

Thamani halisi ya hisa (Intrinsic Value) haijulikani kisahihi, hivyo watu wanaonunua au kuuza hisa hizo hawana uhakika kama bei inalingana na thamani. Intrinsic Value ya hisa inategemea na utendaji wa kampuni husika. Perceived Value inategemea na mtazamo wa soko la hisa kwa ujumla wake.

Kufuatilia mwenendo wa bei ya hisa sokoni ni sawa na kufuatilia Perceived Value ya hisa. Ni sawa na kutaka kujua wanunuzi na wauzaji wa hisa wana mtazamo gani kuhusu hisa za kampuni fulani. Ukweli ni kwamba mtazamo wa washiriki wa soko ni tofauti na utendaji wa kampuni. Ni vitu viwili tofauti kabisa.

Sisi kama wawekezaji tunataka kujikita katika kufuatilia utendaji wa kampuni ili tuweze kukadiria Intrinsic Value kwa usahihi zaidi. Zoezi hili ni endelevu, na tunalifanya mara kwa mara. Tunasoma machapisho mbalimbali, tunafuatilia uchumi wa nchi, tunasikiliza taarifa za kifedha. Tunaendelea kujifunza kuhusu utendaji wa kampuni.

Unaponunua hisa kutokana na ulichokiona katika mwenendo wa bei, hapo ni kwamba hisia zako zinataka kuathiri maamuzi yako. Ni kweli kuna kampuni kadhaa ambazo zimekuwa na mwenendo mzuri wa bei katika soko la hisa. Lakini kutamani kuwekeza katika kampuni hizo kwa sababu ya mwenendo wa bei ya hisa ni kutafuta namna ya kuongeza mawazo.

Endapo utendaji wa kampuni unaridhisha, Perceived Value ya hisa za hiyo kampuni itaakisi kitu hicho. Lakini hapa tunasema "vice versa is not true." Mtazamo wa soko kuhusu thamani ya hisa hauna athari katika utendaji wa kampuni. Hii ndio hoja ya msingi juu ya kuamua kutumia muda mwingi kufuatilia utendaji wa kampuni badala ya mwenendo wa bei ya hisa.

Unatakiwa kuwa na uwezo wa kununua hisa na kuwa na amani hata usipojua tena kuhusu bei ya hisa hizo. Kununua hisa ni kumiliki sehemu ya kampuni. Fuatilia utendaji wa kampuni, sio utendaji wa hisa zake. Vinginevyo unaweza kujikuta kila siku unawaza kupanda na kushuka kwa bei ya hisa. Hilo ni tatizo.

Ukweli ni kwamba hatuna uwezo wa kutabiri Perceived Value ya hisa, kwa sababu hatujui mawazo ya watu wengine yatabadilika vipi. Ukinunua hisa kwa kuamini bei ya hisa itapanda, umeamua kuweka rehani hisia zako ili soko lijue cha kufanya, aidha kukupa huzuni ama furaha.

Hatukatai kwamba kupanda kwa bei ya hisa huleta tija katika uwekezaji. Hoja yetu ya msingi, sisi kama wawekezaji makini, ni kwamba tunatakiwa kujikita katika kufuatilia utendaji wa kampuni badala ya mwenendo wa bei ya hisa za kampuni husika.

Kabla sijamaliza andiko hili, nina swali kwako msomaji. Mara ya mwisho kufuatilia bei ya hisa unazomiliki ilikuwa lini? Je, lengo la kufuatilia lilikuwa nini?

Kwa sasa nimefika ukingoni mwa mbio hizi. Andiko hili ni sehemu ndogo sana, lakini linaweza kufaa kuongeza maarifa kuhusu uwekezaji. Tutakutana wakati mwingine ili tuzidi kujifunza pamoja. Karibu sana.