Ukingo wa Usalama (Margin of Safety).

Ukingo wa Usalama (Margin of Safety).
Margin of Safety

Karibu sana katika blog yetu. Karibu tena tuendelee kujifunza. Siku ya leo tutajifunza kiundani zaidi kuhusu ukingo wa usalama, yaani "margin of safety."

Ukingo wa usalama ni kipimo cha kutumika katika kujua thamani halisi ya hisa (Intrinsic Value) imetofautiana kiasi gani na bei ya hisa sokoni (Share Price). Lengo lake ni kukadiria kiwango cha usalama wa mtaji endapo bei ya hisa itabadilika.

Dhana hii inatumika kwa sababu hatuna uhakika kama thamani halisi ya hisa ni sahihi. Endapo thamani halisi ya hisa ni tofauti na tuliyopata, tunataka kukadiria tutakuwa salama kiasi gani. Tunataka kujua hata ikitokea bei ya hisa ni kubwa, tuna usalama kiasi gani kabla ya mtaji wetu kuanza kupotea? Hii ni dhana ya "break even." Break even hutokea endapo bei ya hisa sokoni inalingana na thamani halisi ya hisa.

Katika kukokotoa margin of safety tunatoa bei ya hisa kwenye thamani halisi ya hisa, kisha tunagawanya na thamani halisi ya hisa. Jibu linalopatikana tunabadili kuwa asilimia.

Kwa mfano thamani halisi ya hisa ni TZS. 750 na bei ya hisa sokoni ni TZS.600, ambapo tukitoa tunapata tofauti ya TZS. 150. Baada ya hapo tunagawanya TZS.150 kwa TZS. 750, tunapata 20%. Kwahiyo margin of safety ni 20%.

Kwa kuwa tumepata margin of safety ambayo ni chanya (positive margin), inaashiria kwamba kuna kiwango cha usalama wa mtaji wetu. Endapo tungepata jibu hasi (negative margin), tafsiri yake ingekuwa kwamba kuna hatari kubwa katika kuamua kuwekeza.

Thamani kubwa ya margin of safety ni bora zaidi kuliko thamani ndogo, kwani huashiria kwamba kiwango cha usalama ni kikubwa zaidi. Muda wote tunakuwa tunajiuliza, ikitokea mtiririko wa fedha unaotarajiwa (future cash flows) ni kidogo zaidi ya makadirio yetu, tuna usalama kiasi gani? Ikitokea mtiririko wa fedha umeshuka, tuna ahueni kiasi gani kabla ya kufikia break even?

Kwa upande mwingine, margin of safety ikiwa hasi inaashiria hali ya hatari. Hapa inakuwa inaonesha kiwango cha hatari iliyopo mpaka kufikia break even. Hapa tunapata jibu la swali : kwa mtiririko wa fedha unaotarajiwa, tunahitaji kuongeza mapato kwa kiwango gani ili kuweza kufikia break even? Hapa tunajaribu kujinasua toka katika hasara ili kurudisha mtaji.

Sisi kama wawekezaji hatutaki tuwe na negative margin of safety, kwa sababu hatuna uwezo mkubwa wa kuathiri utendaji kazi wa kampuni. Wengi wetu ni wamiliki lakini sio waendeshaji wa kampuni. Ni bora kuwekeza katika kampuni ambayo ina positive margin of safety.

Kwa kusema hivyo naomba kusitisha uandishi kwa sasa, ili kuruhusu nafasi ya mambo mengine. Kuna mengi ya kujifunza, na safari inaendelea. Tukutane wakati mwingine ndugu msomaji.

Read more