Umuhimu wa Subira Katika Uwekezaji.

Umuhimu wa Subira Katika Uwekezaji.
Umuhimu wa Subira Katika Uwekezaji

Habari ndugu msomaji. Karibu tena katika blog yetu tujifunze zaidi. Siku ya leo tutaangalia maswala kadhaa kuhusu muda katika uwekezaji, na kupata kuelewa zaidi umuhimu wa subira. Subira yavuta heri. Subira huleta tija kubwa katika uwekezaji wako.

Unapofanya uamuzi wa kuwekeza huna budi kuchukulia uzito jambo hilo. Manunuzi ya hisa yapaswa kufananishwa na manunuzi ya nyumba ya kuishi, au gari. Mara nyingi mtu hanunui nyumba ya kuishi na kuamua kuiuza baada ya miezi miwili ya kuishi katika hiyo nyumba. Mtu huyu anafikiria sanasana jinsi gani ataweza kuiboresha zaidi nyumba yake, na hawazi kuhama hivi karibuni.

Sio hisa pekee, bali hata mali nyingine ambayo utaamua kununua yapaswa kuchukuliwa hivyo. Fikiria kumiliki mali fulani kwa kipindi kirefu. Usiingiwe na tamaa ya kuingiza faida ndani ya muda mfupi ukajikuta unaharibu uwekezaji wako.

Hasara kubwa ya kumiliki mali kwa muda mfupi kisha kuamua kuuza ni makato ya aina mbalimbali. Kuna makato ya kodi ya zuio, makato ya udalali (brokerage fees), makato ya kuhamisha pesa (transaction charges), makato ya kodi ya ongezeko la thamani, nakadhalika. Kama una tabia ya kununua mali na kuimiliki kwa muda mfupi tu, unapoteza sehemu kubwa ya pesa kwa njia hizi. Hii ni changamoto ambayo hatuna budi kuikabili ili kuongeza tija katika uwekezaji wetu.

Licha ya makato hayo, kumiliki mali kwa muda mfupi kisha kuamua kuuza huharibu mtiririko wa riba ambatani (compound interest) uliokuwepo awali. Ukiuza vipande unavyomiliki itakulazimu uanze upya na hautaweza kupata faida iliyopotea.

Chukulia mfano wa kuwekeza katika vipande shilingi laki moja kwa miezi 12 kwa riba ya 1% kila mwezi. Tukiondoa athari ya mfumuko wa bei, uwekezaji wako utakuwa na thamani ya TZS. 112,682.5 baada ya miezi 12. Endapo mtu ameshindwa kusubiri kwa miezi 12 akauza vipande vyake baada ya miezi sita, thamani ya uwekezaji itakuwa TZS. 106,152.02 ambayo itapungua zaidi wakati wa kutoa. Hata akiamua kuanza upya, miezi sita mingine italeta ongezeko la TZS. 6,152 tu. Hii inamaanisha kwa miezi 12 atakuwa amepata faida ya TZS. 12,304 kulinganisha na mtu aliyesubiri miezi 12 ambaye atakuwa amepata faida ya TZS. 12,682.5 katika mtaji uleule wa laki moja.

Unaweza kuhisi tofauti hizo ni ndogo. Kama hapo juu tofauti ya faida "inaonekana" ni TZS. 378.5 tu. Lakini kama mtaji ni mkubwa, tofauti itakuwa kubwa zaidi. Kingine ni makato wakati wa kutoa pesa. Huyu mwekezaji wa miezi sita atakuwa na makato mara mbili au zaidi kulinganisha na mwekezaji wa miezi 12.

Kitu kingine cha msingi hapo ni kwamba uwekezaji wa kununua na kuuza mara kwa mara sio tafsiri halisi ya uwekezaji. Huo unaitwa "ulanguzi." Unaanza kutumia muda wako wa ziada kuhangaika kuuza na kununua mali badala ya kuwa mwekezaji. Kama una shughuli nyingine za kufanya, ulanguzi wa aina hii utasababisha upotevu wa muda.

Hoja ya kuongezea hapa ni kwamba, hata kama unaona thamani ya uwekezaji wako imeongezeka kwa kasi, hiyo pesa ukiitoa inaweza kuisha hata bila kufanyiwa chochote cha maana. Kwa nini usisubiri na kuiacha iendelee kuongezeka zaidi? Endapo kuna dharura imetokea, ni sawa kuuza sehemu ya mali zako. Lakini tofauti na hapo, ni heri kuuacha mtaji wako uendelee kuzalisha faida zaidi.

Natamani sana ikumbukwe kwamba subira italeta tija kubwa kuliko kufanya ulanguzi wa mali. Kama umedhamiria kuwa mwekezaji, fuata misingi ya uwekezaji. Vinginevyo utapoteza rasilimali zako. Subira itakuepusha na mambo mengi.

Yapo mambo mengi sana ya kujifunza, lakini kwa sasa tuishie hapo. Ni vizuri kutumia maarifa haya ili kuona kama kweli yana manufaa yoyote. Tukutane wakati mwingine ili tuendelee kujifunza pamoja kuhusu uwekezaji. Karibu sana.

Read more