Unamiliki Nini?

Unamiliki Nini?
Unamiliki Nini?

"Pesa sio mali." "Kumiliki ardhi ni utajiri." Na misemo mingine. Leo tutajadili kuhusu "mali" katika muktadha wa kifedha.

Kwanza kabisa tuwe na angalizo kuhusu maneno yanayovuma mitaani, mitandaoni, nk. Tuwe makini na "public opinion." Mambo ya kifedha yana tabia ya kubadilika kulingana na wakati, mazingira, elimu, nakadhalika. Mtu mmoja akitamka "pesa sio mali" haina maana ni kweli kwamba pesa sio mali. Ukiambiwa "kumiliki ardhi ni utajiri" haina maana kumiliki ardhi sehemu yoyote kutakupatia tija.

Kulingana na kanuni za kifedha, mali ni kitu chenye uwezo wa kuongezeka thamani (bei) muda unavyozidi kwenda. Ninapomiliki ardhi, inawezekana kuongezeka thamani. Lakini inategemea eneo langu liko wapi, ninafanyia shughuli gani, nilinunua lini na kwa bei gani, nk. Hata kama ardhi ina "uwezo" wa kuongezeka thamani, sio mara zote ardhi huongezeka thamani. Kama umenunua shamba la ekari moja kwa shilingi milioni hamsini, je utaweza kuliuza kwa bei kubwa zaidi, au kulitumia kuzalisha pesa zaidi ya milioni hamsini?

Ukitaka kuelewa zaidi kuhusu mali, angalia watoaji mikopo katika mabenki. Wakati wa "kuthaminisha mali," unaweza ukabaini kwamba kuna kitu chako ulichoamini kuwa ni "mali" kumbe hakijaongezeka thamani kulinganisha na ulipokinunua. Si ajabu kwamba kitu hicho kimeshuka thamani! Mtu akiwa na hatifungani za serikali atapewa kipaumbele kuliko hata mtu anaemiliki nyumba. Unapoamua kununua kitu unachodhani kuwa ni mali, jipe muda wa kutafakari. Tafsiri halisi ya kununua mali ni "uwekezaji."

Kutokana na kufikiria "juu juu," unaweza kuwa na akiba chungu nzima na ukanunua kitu ambacho hakina tija kubwa, ama hakina tija kabisa. Maajabu yake ni kwamba kumiliki mali inayozalisha hauhitajiki kuanza na "mtaji" mkubwa. Ukifikiria kwa mapana zaidi, utagundua kwamba mtu anaweza kumiliki "hisa" na akapata tija kubwa zaidi ya mtu anaemiliki ardhi. Mara nyingi ardhi yenye tija inauzwa bei ghali. Kwa upande mwingine, naweza kumiliki hisa za CRDB hata nikianza na pesa kidogo chini ya shilingi elfu kumi za kitanzania.

Unaweza kupata ardhi porini kwa shilingi elfu hamsini. Ni bei ndogo. Lakini mpaka hiyo ardhi iongezeke thamani, kuna jitihada zitahitajika. Leo hii naweza nikanunua hisa kwa elfu hamsini kisha nikaziuza baada ya muda kwa bei kubwa zaidi, bila kufanya jitihada zozote.

Kama ulinunua ardhi nje ya mji, na baada ya miaka kadhaa kukawa na maendeleo katika hilo eneo, ni dhahiri kuwa mali yako itakuwa na tija kubwa. Kitu muhimu hapa na katika uwekezaji kwa ujumla ni "muda." Kitu kingine ni kufanya utafiti kabla ya kununua "mali." Kiukweli inaweza ikawa ngumu kutabiri kwamba ardhi itapanda thamani kama umenunua shamba kijijini na kuliacha bila kufanyia chochote.

Mtu mmoja alikopa shilingi milioni mia moja akajenga nyumba ya kupangisha. Kodi kwa mwezi analipwa jumla shilingi milioni moja. Kwa mwaka mmoja analipwa milioni 12. Mtu mwingine akaona usumbufu kuanza kujenga na kuhangaika na wapangaji. Yeye akatumia hiyo milioni mia moja kununua hatifungani za serikali za miaka 25, zenye riba (coupon rate) ya 15.95% kwa mwaka. Kwa mwaka mmoja analipwa zaidi ya milioni 15 bila kufanya chochote. Hapa kila mmoja amepata tija kutokana na mali anayomiliki. Lakini huenda mmiliki wa nyumba angeweza kupata tija kubwa zaidi.

Lengo kubwa sio kukwepa kumiliki aina fulani ya mali. Lengo ni kupanua wigo wa fikra kabla ya kununua mali. Ni muhimu kumiliki mali za aina tofauti tofauti. Lakini pia ni muhimu kufanya utafiti kila unapoamua kufanya hivyo. Pesa za kigeni (foreign currency) ni mali. Pesa za kidigitali (cryptocurrency) pia ni mali. Tutafute sana maarifa.

Kwa leo tuishie hapo. Wakati ujao tutazidi kujifunza juu ya maswala mbalimbali ya fedha na uwekezaji. Swali la leo ni kwamba, mtu anaemiliki biashara anaweza kusema kuwa biashara yake ni mali? Kama jibu ni ndiyo, ni katika misingi gani biashara inaweza kuwa mali?

Read more