Upatu Haramu (Pyramid Scheme).
Siku ya leo tutajifunza kuhusu upatu haramu kwa kuangalia maana yake, sifa zake, sheria ya Tanzania kuhusu upatu haramu, tahadhari za kuchukua, na mengine.
Upatu ni utaratibu wa kuchangiana pesa miongoni mwa wanachama waliojiunga. Upatu unaweza kuwa halali ama haramu, kulingana na kwamba sheria za nchi zimezingatiwa au la. Vipo vyama vingi vyenye sifa za kuitwa upatu, lakini vingine vinakiuka sheria na hivyo kupewa jina la upatu haramu. Kwa kiingereza upatu haramu unajulikana kama pyramid scheme au Ponzi scheme. Jina la Ponzi scheme lilitokana na muitaliano Charles Ponzi, ambaye aliwatapeli watu kupitia upatu haramu mwaka 1920 na akawa milionea kupitia njia hiyo.
Upatu haramu ni mpango wa kuchangisha pesa za watu kwa ahadi ya kupata faida kubwa ndani ya muda mfupi, bila jitihada zozote kwa upande wa mchangiaji. Mchangiaji mara nyingi hushawishiwa kuwashawishi na watu wengine wajiunge katika mpango huo. Mchangiaji anaahidiwa kulipwa faida hata mara mbili au zaidi ndani ya muda mfupi, kitu ambacho asingeweza kufanikisha kwa njia nyingine yoyote katika uhalisia. Uhalisia unapinga uwezekano wa kuingiza faida kubwa ndani ya muda mfupi KIHALALI. Mtu ataambiwa maneno mengi ya ushawishi, kwa lengo la kucheza na hisia za tamaa (greed) na hata hofu (fear).
Kwa kawaida binadamu hana uwezo wa kufanya maamuzi bora anapokuwa katika hali ya hisia kali kama vile furaha iliyopitiliza, hasira, huzuni, matumaini makubwa (unrealistic optimism), au hofu. Waanzilishi wa upatu haramu pamoja na matapeli wengine wanatumia udhaifu huu kupata pesa nyingi kiasi cha kuwa mamilionea!
Zifuatazo ni baadhi ya sifa za upatu haramu. Zingatia sifa hizi ili ujue kama "unapiga" pesa au "unapigwa" mwenyewe.
- Ahadi ya faida kubwa bila kubainisha itazalishwa kwa njia gani.
- Hakuna waraka wa matarajio (prospectus) wa kuonesha mpango huo utaendeshwa vipi.
- Mchangiaji mpya anahamasishwa kuwashawishi na wengine wachangie.
- Kutokuwa na idhini ya mamlaka husika kama vile CMSA (Capital Market and Securities Authority).
- Waendeshaji kutumia mifano ya baadhi ya watu waliofanikiwa kupitia mpango husika ili kukufanya uamini kwamba hata wewe unaweza "kufanikiwa!"
- Kukosekana kwa mkataba wa kujiunga au kurudishiwa pesa endapo mpango ukifeli.
- Hakuna mradi maalumu wa kuwekeza pesa wanazochanga watu. Kama kuna mradi, utatajiwa jina bila kupewa maelezo ya kina.
- Mapato yanatokana na pesa wanazochangia wanachama wapya. Pesa hizo ndio zinakuwa "faida" ya kuwalipa wachangiaji wa awali.
Tuchukulie mfano nakuahidi nitakulipa mara mbili ya mtaji ndani ya wiki tatu. Labda nikasema unatakiwa kuanza na mtaji wa TZS. 200,000. Tafsiri yake ni kwamba natakiwa nikulipe wewe TZS. 400,000 baada ya wiki tatu kupita. Ili niweze kukulipa itabidi wapatikane wachangiaji wawili wapya ndani ya hizo wiki tatu, kila mmoja atoe TZS. 200,000 kisha nikulipe wewe. Kama ndani ya hizo wiki nitashindwa kuwa na wachangiaji wapya, nitakuwa sina namna yoyote ya kukulipa hata ile TZS. 200,000 ya mwanzo! Hii ni kwa sababu hata hiyo TZS. 200,000 itakuwa imeshatumika kuwalipa wachangiaji wa kabla yako. Ili mambo yaende vizuri inabidi nikuhamasishe kuwaleta wachangiaji wengine, kwa sababu "kizuri kula na mwenzio!" Ikitokea hakuna tena wachangiaji wapya, napotea bila taarifa yoyote, na pesa yako inakuwa imekwenda.
Kulingana na Sheria za Kanuni na Adhabu (Penal Code Cap 16 Sect 171A), ni kosa la "jinai" KUENDESHA, KUSHIRIKI, KUCHANGIA au KUSHAWISHI WENGINE KUCHANGIA pesa katika upatu haramu. Licha ya kushiriki katika kupoteza pesa zako mwenyewe, unashiriki katika kosa la jinai! Yani kupoteza pesa ni pigo, lakini unapoteza pesa na kuvunja sheria kwa wakati mmoja. Hii ni mbaya kuliko.
Chukua tahadhari zifuatazo ili uweze kuepuka kupoteza pesa na kuvunja sheria kwa kuchangia katika upatu haramu.
- Omba waendeshaji wa mpango husika wakupatie waraka wa matarajio (prospectus) uliopitishwa na CMSA. Kama hawana waraka huo, hawana idhini ya kuchangisha pesa kutoka kwa watu.
- Ongea na watu wako wa karibu ili kujua kama wamewahi kusikia kuhusu "fursa" hiyo adimu. Kuna muda watu wanatapeliwa kwa sababu wanashindwa kuongea na marafiki kuuliza kuhusu mambo haya.
- Fuatilia historia ya mpango huo wa upatu. Kama ni mpango mpya, kuwa makini sana. Kama wanasema walianza muda mrefu, omba wakupatie nyaraka muhimu kuonesha utendaji kazi wa miradi yao.
"Kama mtu anakushawishi sana kujiunga na fursa, jua kuwa wewe mwenyewe ndio fursa." Matapeli wanaona kuna fursa katika kutumia udhaifu wako ili wapate pesa zako kiurahisi. Ni heri upoteze pesa kwa njia halali, sio kupoteza pesa kwa njia haramu, tena wakati ambapo ulidhani unafanya "uwekezaji."
Natumaini mpaka sasa tunayo picha nzuri juu ya upatu haramu. Tuendelee kujifunza pamoja, kwa sababu kuna muda unaweza kujitenga ukaingia matatizoni. Usiamini sana akili yako kiasi cha kushindwa hata kuwauliza wengine kuhusu vitu hivi. Tukutane tena wakati ujao kwa elimu zaidi.