Uwekezaji Endelevu.
Karibu tena tuendelee kujifunza kuhusu uwekezaji. Mwekezaji sio mtu anayemiliki mali pekee, bali pia ni mtu mwenye jitihada endelevu za kutafuta kumiliki mali zaidi. Ni mtu mwenye "utamaduni" wa kuwekeza. Ni mtu anayefuatilia fursa za uwekezaji muda wote, bila kujali ana kipato gani kwa wakati huo. Ukweli ni kwamba bila kuwa na utamaduni wa kuwekeza, ni ngumu kupata tija kutokana na uwekezaji wako.
Katika andiko la leo tutajaribu kuangalia umuhimu wa uwekezaji endelevu. Kama mtu anafanya kazi na kulipwa pesa kila mwezi, inaashiria kwamba mtu huyu ana uwezo wa kuweka akiba kila mwezi pia. Kama ni hivyo, kuna haja ya kuendeleza utaratibu wa kufuatilia fursa za kuwekeza kila mwezi pia. Huenda akiba iliyopo bado haitoshelezi kuanza aina fulani ya uwekezaji, lakini hicho kisiwe kisingizio cha kuacha kufuatilia fursa za uwekezaji. Vinginevyo inakuwa rahisi sana kuingia katika mtego wa kungojea kuwa na mtaji mkubwa ilhali hujui utawekeza wapi.
Kitu kingine kuhusu uwekezaji endelevu ni kwamba unapofanya uwekezaji mara nyingi inasaidia kuongeza thamani ya uwekezaji wako zaidi. Sambamba na kupanda kwa thamani ya mali, uwekezaji zaidi husaidia kukuza mtaji wako. Kama mwanzoni ulinunua hisa 80 za kampuni, zitakuwa zinaendelea kupanda thamani, lakini idadi yake itabaki kuwa hisa 80 zilezile. Endapo una utaratibu wa kununua hisa 40 kwa mwezi, idadi ya hisa zako itakuwa inaongezeka pia. Huu ni uthibitisho kwamba kuwekeza mara kwa mara husaidia kukuza thamani ya mtaji uliowekezwa.
Kitu kingine cha kuzingatia hapa ni kwamba hatuwekezi faida tu, bali tunaendelea kutumia akiba iliyopo kuongeza uwekezaji. Unawekeza gawio ulilopata. Unawekeza pia sehemu ya akiba iliyopo kutokana na pesa ulizopata katika kipindi fulani.
Faida ya uwekezaji endelevu ni kwamba itasaidia kupambana na mfumuko wa bei kwa kanuni iitwayo "dollar cost averaging." Hata ikitokea pesa ulizowekeza mwanzoni zimeshuka thamani kwa sababu ya mfumuko wa bei, uwekezaji endelevu husaidia kwa sababu utakuwa unawekeza pesa kulingana na thamani halisi ya pesa kwa wakati husika. Chukulia mfano wa kuwekeza laki mbili mwaka 2024 mwanzoni kisha kuiacha bila kuwekeza tena kiasi chochote. Kutokana na athari ya mfumuko wa bei, sehemu fulani ya hiyo laki mbili itapotea. Endapo mtu mwingine aliwekeza laki moja 2024 mwanzoni, kisha kuwekeza laki moja nyingine baada ya miezi mitatu, atakuwa ameweza kupunguza upotevu wa thamani katika mtaji wake.
Endapo mfumuko wa bei ni 1% kwa mwezi, laki mbili itakuwa na thamani ya TZS 188,296.03 baada ya miezi sita. Ukiwekeza kwa awamu mbili laki moja kila miezi mitatu, baada ya miezi sita thamani ya mtaji wako itakuwa TZS. 191,177.91 ambayo ni kubwa zaidi. Hapa inatumika kanuni ya riba ambatani lakini riba inakuwa hasi na sio chanya. Hii ndio nguvu ya uwekezaji endelevu.
Cha kujifunza hapa ni kwamba ni busara kuwa na utaratibu wa kuwekeza mara kwa mara. Usiwekeze mara moja tu. Ukiweza kufanya uwekezaji kila mwezi itakuwa vizuri zaidi. Lakini ukishindwa kufanya hivyo angalia kinachowezekana kutekelezwa kwa upande wako. Licha ya kupunguza athari za mfumuko wa bei, uwekezaji endelevu huongeza thamani ya uwekezaji wako. Kanuni hii ikitumika pamoja na kanuni ya riba ambatani, mtaji unaweza kuongezeka thamani vizuri sana.
Kwa sasa tuishie hapo. Ni imani yangu kwamba mambo haya yanaeleweka vyema. Ni imani yangu kwamba mambo haya yakifanyiwa kazi yataleta tija zaidi katika uwekezaji wako. Ni vyema kuyafanyia kazi ili kuona ufanisi wa kanuni hizi. Tutakutana wakati mwingine ili tuendelee kujifunza. Karibu sana.