Uwekezaji Katika Thamani (Value Investing).
Ni wakati mwingine tena nimepata nafasi ya kuandika. Karibu tena tuendelee kujifunza. Siku ya leo tutajifunza dhana ya uwekezaji katika thamani (Value Investing), ambayo ni falsafa muhimu sana ya uwekezaji. Kuna namna nyingi za kuwekeza, kulingana na mitazamo tofautitofauti.
Value Investing inalenga kuwekeza pesa katika biashara zenye uwezo mkubwa wa kutengeneza tija (Value) siku zijazo, ambapo tunalenga kununua hisa za kampuni husika kwa bei nafuu. Hivyo tuna pande kuu mbili za kuangalia. Kuna upande wa kuchambua kampuni (analyzing the company), na upande wa kuthaminisha hisa (share valuation).
Katika maandiko kadhaa tulijaribu kugusia kiufupi kuhusu mchakato wa uchambuzi wa kampuni na hisa kwa ujumla (security analysis). Falsafa ya Value Investing ni kama muongozo ambao unatoa msingi wa vitu vya kuzingatia unapotaka kuwekeza katika kampuni fulani.
Kulingana na kanuni za Value Investing, tunataka kuwekeza katika kampuni yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na ushindani katika biashara. Kampuni yenye mtiririko mzuri wa fedha (cash flow). Kampuni ambayo imeweza kuwa na utendaji kazi bora kwa miaka mingi (consistent performance). Kampuni yenye uwezo mkubwa wa kulipia gharama za uendeshaji na kubakiwa na kiasi kikubwa cha fedha (free cash flow).
Kingine tunachoangalia ni ubora wa mfumo wa uongozi (management system) wa kampuni. Kiufupi ni kwamba uongozi bora unaleta matokeo bora kwa wawekezaji. Tunaangalia viongozi wakuu wa kampuni wanalipwa mishahara kwa viwango gani na kwa vigezo gani. Je, kuna matumizi ambayo sio ya lazima yanafanyika? Kama kuna dalili zozote za udhaifu katika uongozi wa kampuni, ni muhimu kuwa makini. Viongozi wengi wapo kwa ajili ya maslahi binafsi, ambayo huenda hayalingani na maslahi ya wawekezaji.
Kitu kingine katika Value Investing ni thamani ya hisa. Hata biashara iwe inafanyika vizuri kiasi gani, bei ya kununulia hisa inaweza kuathiri tija utakayopata kwa kiwango kikubwa. Tunaangalia thamani ya hisa kulingana na utendaji wa kampuni (Intrinsic Value). Thamani ya hisa katika soko (Share Price) haifanani na thamani ya hisa kulingana na utendaji wa kampuni. Lengo katika Value Investing ni kutafuta kampuni ambazo zina "Share Price" ndogo kulinganisha na "Intrinsic Value" yake. Kufanya hivyo husaidia kupunguza hatari katika uwekezaji. Lakini pia inasaidia kuongeza tija inayoweza kupatikana katika uwekezaji (investment return).
Share Price ikiwa ndogo kulinganisha na Intrinsic Value inasaidia kuwa na thamani kubwa ya Ukingo wa Usalama (Margin of Safety). Dhana hii ni ya msingi sana katika uwekezaji wako. Soko la hisa lina kiwango kikubwa cha hatari (high risk). Hata kama kampuni inafanya vizuri, haina maana ukinunua hisa zake utapata faida kubwa.
Mwenendo wa bei ya hisa hutegemea mitazamo (sentiment) ya wawekezaji katika soko. Kama wanaamini kampuni itafanya vizuri (optimistic) bei ya hisa itapanda. Kama wanaamini kampuni itafanya vibaya (pessimistic) bei ya hisa itashuka. Ukinunua hisa kwa bei kubwa kulinganisha na Intrinsic Value, unajiweka katika hatari kubwa kutokana na mabadiliko haya ya bei katika soko la hisa.
Intrinsic Value inaweza kupatikana kwa kufuata njia nyingi tofauti. Njia mojawapo inajulikana kama DISCOUNTED CASH FLOW MODEL (DCF). Ni njia ya makadirio, na haiwezekani kupata kwa usahihi thamani ya kweli ya hisa. Umuhimu wa kukokotoa Intrinsic Value ni kwamba inasaidia kuongeza umakini katika kuzingatia utendaji wa kampuni na sio kuangalia mwenendo wa bei tu.
Dhana ya Margin of Safety pia inasaidia kwa sababu Intrinsic Value sio sahihi. Margin of Safety inakuwa kama ulinzi wako kutokana na kutokuwa na uhakika juu ya thamani halisi ya hisa. Kuna namna ya kukokotoa Margin of Safety, ambayo sio ngumu. Hata hivyo, katika andiko la leo hatutagusia mahesabu hayo.
Tunapochambua kampuni tunajikita pia kuangalia uwezo wa kampuni kuzalisha faida kubwa kutokana na mali zilizopo. Tunaangalia mapato ya kampuni. Tunaangalia kiwango cha ukwasi (liquidity), na vitu vinginevyo.
Kutokana na umuhimu wa dhana nzima ya Value Investing, andiko hili ni kama utangulizi tu. Tutazidi kuangalia kiundani kuhusu dhana hii. Uwekezaji ni sayansi na sanaa kwa wakati mmoja. Mtu anaweza kufanya uchambuzi wake na akapata majibu tofauti na wengine. Endapo utatumia kanuni bora za uwekezaji, tija itapatikana hatimaye.
Kwa sasa tuishie hapo. Tutaendelea kujifunza wakati mwingine kulingana na nafasi itakayopatikana. Tunajikita zaidi katika soko la hisa kwa sababu huko ndiko kwenye sintofahamu zaidi. Lakini pia ndiko kwenye uwezekano mkubwa zaidi wa kutengeneza faida kubwa. Nakutakia heri katika uwekezaji wako. Wakati mwingine tutaendelea.