Washauri wa Uwekezaji.

Washauri wa Uwekezaji.
Washauri wa Uwekezaji

Ni wakati mwingine tena tuliopata kwa ajili ya kuendeleza elimu ya uwekezaji. Siku ya leo tutaangalia vitu kadhaa kuhusu washauri wa uwekezaji. Ni wazi kwamba mara kwa mara tunahitaji ushauri kabla ya kufanya maamuzi. Hata katika upande wa uwekezaji kuna haja ya kutafuta ushauri kabla ya kuamua kuwekeza.

Ili kuweka mambo sawa, nataka kutoa tafsiri ya neno "ushauri" kama linavyotumika katika andiko hili. Tunaposema ushauri tunamaanisha maoni ya mtu mwingine juu ya wapi uwekeze pesa zako ili kupata tija zaidi. Ni maana ambayo sio pana, na imejikita upande huo tu. Tungeweza kufafanua kwa namna nyingine, lakini maana iliyotolewa inafaa zaidi kwa matumizi yetu katika andiko hili.

Kwa sababu hatuna uhakika tuwekeze wapi, tunaamua kuomba ushauri kwa watu wengine. Ni jambo zuri, lakini kuna haja ya kuzingatia mambo kadhaa. Kitu cha kwanza kuzingatia ni kwamba kuna washauri wa uwekezaji wanaotambulika kisheria, kulingana na mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA). Endapo unataka kuomba ushauri ili kuwekeza katika masoko ya mitaji au masoko ya fedha, tafuta ushauri kutoka kwa watu hao.

Miongoni mwa washauri wanaotambulika kisheria ni madalali wa soko la hisa DSE. Wengineo ni taasisi kama UTT AMIS, nakadhalika. Kuwa huru kupiga simu kwao ili kupata ushauri kulingana na uhitaji wako. Kadiri ya malengo uliyonayo, pamoja na vitu vinginevyo kama vile umri na kipato chako, utapata ushauri unaoweza kukusaidia kufanikiwa katika uwekezaji wako.

Jambo lingine kuhusu ushauri wa uwekezaji ni kwamba, usitegemee ushauri bila kufanya jitihada za kutafakari wewe mwenyewe. Usemi wa, "akili ya kuambiwa changanya na yako" unafaa sana katika muktadha huu. Hata kama washauri wa uwekezaji ni wataalamu, hawapo sahihi wakati wote. Isitoshe pesa ni za kwako mwenyewe. Sasa kwanini unataka kuchukua ushauri kama ulivyo bila kutafakari? Ikitokea hasara utamlaumu nani?

Kulingana na aya iliyopita, tunaona kwamba kuna haja ya kuwa na uelewa kiasi fulani juu ya uwekezaji, badala ya kutegemea "wataalamu" pekee. Ikumbukwe kwamba hata wao na utaalamu wao huwa wanapata hasara katika uwekezaji. Ni vyema kujifunza mbinu za uchambuzi wa kifedha walau kidogo, kuliko kutokujua kitu kabisa.

Sisi kama wawekezaji tuna wajibu wa kufuatilia kuhusu uwekezaji kwa sababu ni wazi kwamba tumetumia nguvu kubwa kutafuta na kutunza pesa. Hatuwezi kukubali kuruhusu uzembe wakati wa kuwekeza. Sio kwamba tutazuia uwezekano wa kupata hasara, la hasha. Lakini kufanya hivyo itasaidia kuongeza uwezekano wa kufanikiwa katika uwekezaji wetu.

Kitu kingine kuhusu ushauri wa uwekezaji ni kwamba tusitegemee ushauri wa watu wengi kupita kiasi. Ikiwezekana sikiliza ushauri wa mtaalamu mmoja tu. Unapozidi kusikiliza ushauri unapunguza hali ya kujiamini, na unaweza hata kukosa fursa muhimu kwa kuamini bado hauna uhakika. Ukweli ni kwamba wakati wowote wa kufanya maamuzi hatuwezi kuwa na picha kamili juu ya nini tutarajie. Kuna hali ya sintofahamu ambayo haiwezi kuepukika.

Kwa kusema hayo machache, naamua kutamatisha andiko hili la leo. Sio kwa maana kuwa nimemaliza kila kitu unacho hitaji kujua kuhusu washauri wa uwekezaji, bali ni kwa lengo la kuruhusu nafasi ya mawazo mengine pia. Tutakutana wakati mwingine ili tuzidi kujifunza kuhusu uwekezaji.